Uropokaji mpya wa Trump dhidi ya Iran
(last modified Thu, 13 Jun 2019 11:20:45 GMT )
Jun 13, 2019 11:20 UTC
  • Uropokaji mpya wa Trump dhidi ya Iran

Rais Donald Trump wa Marekani daima amekuwa akichukua misimamo ya chuki na uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni amekuwa akitumia stratijia ya 'mashinikizo ya juu zaidi' kuilazimisha Iran ikubali matakwa yake ya kidhalimu.

Katika uropokaji wake wa hivi karibuni dhidi ya Iran, Trump amekariri madai yasiyo na msingi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono ugaidi na kwamba ndio chanzo cha machafuko na mivutano duniani. Akizungumza na waandishi habari huko White House akiwa na mgeni wake, rais wa Poland, Trump amedai kwamba Iran inaendesha vita na ugaidi katika eneo na katika ngazi za kimataifa. Vilevile amedai kwamba hatua yake ya kuiondoa Marekani katika mapatano ya kimataofa ya JCPOA imepelekea Iran kubadili mwenendo wake na wakati huohuo kuisababisha matatizo makubwa ya kiuchumi. Trump alichukua hatua hiyo tarehe 8 Mei mwaka uliopita na kuanzisha tena vikwazo vya nyuklia vya nchi hiyo dhidi ya Iran.

Tokea aingie madarakani huko Marekani, Trump amekuwa akiituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba imekiuka mapatano ya JCPOA kupitia mpango wake wa makombora, kuvuruga usalama wa eneo na kuunga mkono 'makundi ya kigaidi.' Tuhuma hizo za Trump dhidi ya Jamhuiri ya Kiislamu ya Iran zinatolewa katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni Iran imekuwa na nafasi muhimu sana katika kuyatokomeza makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Iraq na Syria. Daesh na makundi mengine ya kigaidi yalikuwa yameeneza shughuli zao za ugaidi katika nchi mbili hizo kwa msaada na ushirikiano wa karibu wa Marekani na Saudi Arabia.

Trump baada ya kutia saini dikrii ya kuondoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA

Hili ni suala ambalo Trump mwenyewe amelikiri hadharani. Mwezi Januari 2016 alimkosoa vikali rais wa wakati huo wa Marekani Barack Obama pamoja na waziri wake wa mambo ya nje Hillary Clinton kwa kuanzisha na kulifadhili kwa hali na mali kundi hilo la kigaidi. Katika upande wa pili, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni muhanga mkuu wa vitendo vya ugaidi katika eneo, iliamua kupambana vikali na makundi hayo ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekanii na washirika wake katika nchi za Iraq na Syria, na hii ni baada ya ombi rasmi lililowasilishwa kwake na serikali halali za nchi hizo. Ilichangia pakubwa kuyotokomeza makundi hayo kwa kuzipa nchi hizo ushauri wa kijeshi, jambo ambalo daima limekuwa likizichukiza nchi za Marekani, utawala haramu wa Israel na Saudia.

Akizungumza Jumanne usiku huko White House, Trump alidai kuwa Iran imebadili sera zake kutokana na mashinikizo ya serikali yake  na kwamba hivi sasa Iran inakabiliwa na matatizo mengi kutokana na mashinikizo hayo. Amekiri kwamna serikali yake inawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran kutokana na vikwazo vya kiuchumi inavyowawekea. Amesema: thamani ya pesa zao imeshuka kadiri kwamba hawawezi hata kununua mkate mmoja! Amedai kutaka kuisadia Iran kwa kusema: 'Niko tayari kuisaidia Iran kutatua matatizo haya.'

Matamshi ya mgongano na ya kindumakuwili ya Trump kuhusiana na Iran ambapo kwa upande mmoja anadai kwamba Iran inaunga mkono ugaidi na kwa upande wa pili kudai kuwahurumia watu wa Iran, kwa hakika yanadhihirisha wazi hasira kubwa aliyonayo dhidi ya wananchi wa Iran, na hii inatokana na uamuzi wao wa kutoshirikiana naye katika njama zake za kutaka kuiangusha serikali ya Kiislamu ya Iran.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havijakuwa na taathira kubwa

Wananchi wa Iran daima wamekuwa wakionyesha utiifu wao imara na usioterereka kwa mfumo wa Kiislamu wa Iran na wakati huohuo kutangaza kuwa kwao tayari kwa ajili ya kukabiliana vilivyo na njama zozote za Marekani dhidi ya mfumo huu.

Siasa za Marekani dhidi ya Iran zimejengeka katika msingi wa vitisho na utumiaji mabavu. Pampja na hayo lakini Iran katika kipindi cha miaka 40 iliyopita imesimama imara mbele ya siasa hizo za mabavu na hivyo kuzifanya njama hizo za Marekani kutokuwa na taathira zozote za maana.

Kwa mujibu wa kauli ya Trudy Rubin, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Marekani: Ukosoaji wa wazi wa Trump dhidi ya Iran na ombi lake kwa washirika wa Marekani wajiunge na kampeni ya Washington dhidi ya Iran ni dalili inayothibitisha wazi kwamba siasa zake dhidi ya serikali ya Tehran zimefeli. Iran imethibitisha wazi kivitendo kwamba inaweza kuvishinda vikwazo vya Marekani na kukabiliana vilivyo na siasa za uadui na chuiki za serikali ya Trump.

Tags