Katibu Mkuu wa UN: Iran ingali imefungamana na JCPOA
(last modified Fri, 21 Jun 2019 11:29:22 GMT )
Jun 21, 2019 11:29 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Iran ingali imefungamana na JCPOA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

António Guterres amesema katika ripoti kuwa, "Iran haijakengeuka ahadi zake za kufungamana na Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Ameongeza kuwa, "Tathmini yetu imebaini kuwa, Tehran ingali inatekeleza wajibu wake na shughuli zake za nyuklia zinaendana na ahadi zake za makubaliano hayo ya JCPOA."

Licha ya tuhuma zinazotolewa na Marekani kwamba Iran haijatekeleza majukumu wala kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hata imeituhumu nchi hii kuwa inafanya juhudi za kuunda silaha za nyuklia, lakini ripoti ya karibuni ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) inaeleza kuwa, Tehran inaendelea kuheshimu na kutekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Hata hivyo Tehran inasisitiza kuwa muda wa siku 60 ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliupa Umoja wa Ulaya uwe umetekeleza ahadi zake za kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na uache tabia ya kulegalega hautarefushwa.

Kutokana na hali hiyo ya kulegalega nchi za Ulaya katika utekelezaji wa mfumo wa mabidilishano ya kibiashara wa INSTEX, Rais Hassan Rouhani wa Iran tarehe 8 mwezi uliopita alisema kwamba Tehran imesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kukiwemo kuongeza akiba ya urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito ya nyuklia, na kwamba itachukua hatua zaidi iwapo EU haitachukua hatua za kivitendo za kuilinda JCPOA.

Tags