"Siasa za Marekani dhidi ya Iran zimefeli"
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54619-siasa_za_marekani_dhidi_ya_iran_zimefeli
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, siasa za serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimefeli.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 08, 2019 02:42 UTC

Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, siasa za serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimefeli.

Shirika la habari la Fars limemnukuu Sheikh Ali Damush akisema hayo jana (Jumapili) na kuongeza kuwa, ushahidi wa kufeli na kushindwa siasa za Marekani mbele ya Iran uko wazi kabisa kiasi kwamba Washington inashindwa hata kuzuia kuonesha kushindwa na kuchanganyikiwa kwake mbele ya Iran.

Amesisitiza kuwa, njia ya mkato zaidi ya kuleta utulivu na kulinda usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi ni mazungumzo na Iran yaani kufikia maelewano na nchi hiyo na sio kuendesha siasa za vikwazo na mashinikizo.

Sheikh Ali Damush

 

Baada ya kuitoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo tarehe 8 Mei 2018, Donald Trump aliirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo ya kimataifa.

Rais huyo mwanagenzi wa Marekani alitangaza kuwa lengo la vikwazo vyake alivyodai ni vikubwa kupindukia dhidi ya Iran ni kuilazimisha Tehran ifanye mazungumzo mengine yatakayohusu masuala yote yanayotakiwa na Marekani, ikiwemo haki ya kujilinda na kujiimarisha kiulinzi Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni moja ya nguzo kuu za kambi ya muqawama, ndiyo inayotoa mchango mkubwa na wa kimsingi kabisa katika kukabiliana na njama na uadui wa kambi ya Kimarekani - Kizayuni katika eneo hili, suala ambalo linaihamakisha sana Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na vibaraka wao.