Trump atishia kuwaachilia magaidi wa Daesh warejee katika nchi za Ulaya
Marekani imekuwa na nafasi muhimu katika kubuni na kueneza shughuli za makundi ya kigaidi likiweo la Daesh katika mgogoro wa Syria kwa lengo la kuindoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo.
Mbali na hayo, Rais Donald Trump wa Marekani amezitaka nchi za Ulaya ziwapokee magaidi hao wa Daesh. Akizungumza jana usiku, Trump amezitishia nchi hizo kwamba atawaachilia huru magaidi wa Daesh iwapo nchi hizo hazitatekeleza majukumu yao ya kuwarudisha nchini kwao magaidi 2500 wa kigeni waliokamatwa katika nchi za Syria na Iraq. Kwa muda mrefu sasa Rais Trump amekuwa akizikosoa nchi za Ulaya kwa kukosoa kuwarudisha nyumbani magaidi waliokamatwa katika nchi mbili hizo za Kiarabu na kuwahukumu katika nchi zao.
Hii si mara ya kwanza kwa Trump kuzitaka nchi za Ulaya ziwapokee raia wao ambao walienda Syria na Iraq kwa lengo la kujiunga na magaidi wenzao wa Daesh. Mwezi Februari mwaka huu, alizitaka nchi za Ufaransa, Uherumani na Uingereza ziwapokee na kuwahukumu magaidi 800 wa Daesh waliotiwa mbaroni na Marekani nchini Syria. Wakati huo pia Marekani ilionya kwamba ingewaachilia huru magaidi hao iwapo hawengeruhusiwa kurejea katika nchi zao, tishio ambalo lilizikasirisha nchi za Ulaya.
Trump amekuwa akidai mara kwa mara kwamba Marekani imekusudia kuwaangamiza kabisa magaidi wa Daesh na kwamba atawalinda watu dhidi ya magaidi hao wasio na huruma. Madai hayo ya Trump yanaenda kinyume na ukweli wa mambo na kidhahiri amesahau kwamba yeye mwenyewe katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016 alikiri waziwazi kwamba serikali ya Barack Obama wa nchi hiyo ndiyo iliyobuni kundi hilo hatari la kigaidi. Kwa msingi huo ni Marekani ndio mwanzilishi wa kundi hilo la kigaidi.
Ikiongoza muungano wa nchi za Magharibi na Kiarabu katika mgogoro wa Syria mwaka 2011, Marekani ililitumia kundi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi kulinda kufikia malengo yake katika nchi hiyo ya Kiarabu. Akizungumzia suala hilo, Ivan Ipolitov, mtaalamu wa masuala ya siasa anasema, lengo la Marekani katika miaka ya hivi karibuni limekuwa ni kuyatumia makundi ya kigaidi kwa ajili ya kutekeleza siasa zake za nje na matokeo ya jambo hilo ni kuzidhoofisha nchi za Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na kuandaliwa mazingira ya kuenea makundi ya kigaidi na yenye fikra za kupindukia mipaka.
Mtazamo huo inaafikiana kabisa na wa wataalamu wengine wa nchi za Magharibi. Wanasema kwamba nchi za Magharibi zimekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha na kueneza fikra za kigaidi katika pembe mbalimali za dunia kwa ahili ya kufikia malengo yao katika sehemu hizo. Frederic Poisson mtaalamu wa Magharibi wa Masuala ya Asia Magharibi anaamini kwamba Marekani na Ufaransa zimeshirikiana kubuni kundi la Daesh. Kwa msingi huo Ulaya pia imeshirikiana na Marekani katika kubuniwa kwa kundi la Daesh.
Tokea mwaka 2011 hadi 2014 kipindi ambacho Daesh ilikuwa ikiendesha vita vya kutaka kuingusha serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa nchi hiyo, Marekani ilikuwa katika mstari wa mbele wa kuchangia na kulisaidia kwa hali na mali kundi hilo liweze kufikia malengo yake kwa maslahi ya utawala wa Washington. Baada ya kuenea harakati za kigaidi na kitakfiri za kundi hilo katika nchi jirani ya Iraq na kutekwa mikoa kadhaa ya nchi hiyo, ambapo muungano wa kimataifa uliodaiwa kuwa ni wa kupambana na kundi hilo ulibuniwa mwaka 2014, lengo la Marekani lilikuwa ni kulinda utambulisho na harakati za kundi hilo kupitia mfumo maalumu wa udhibiti, ili iweze kulitumia dhidi ya jeshi la Syria na washirika wake.
Kwa kweli madai ya Marekani ya eti kupambana na magaidi wa Daesh ni ya kushukiwa sana. Hivi sasa Trump anazitaka nchi za Ulaya zipokee na kuwahukumu magaidi wa Daesh baada ya kuwatumia kudhamini maslahi yake katika nchi za Syria na Iraq. Baada ya kuona kuwa hawana tena faida kwake, Marekani inazishinikiza nchi za Ulaya ziwapoekee na kuwahukumu ili kuepuka shari yao.