Aug 13, 2019 03:29 UTC
  • Marekani yaanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha bilionea Epstein akiwa jela

Mwanasheria Mkuu wa Marekani amesema kuwa umeanzishwa uchunguzi kuhusu kifo cha kutatanisha cha bilionea aliyekuwa mfadhili na rafiki mkubwa wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo akiwa ndani ya jela ya nchi hiyo.

Gazeti la Independent la Uingereza limeripoti kuwa, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr ambaye pia ni Waziri wa Sheria wa nchi hiyo ametangaza kuwa, Mkaguzi Mkuu wa Wizara hiyo ataanzisha uchunguzi kuhusu mazingira yaliyoandamana na kijinyonga kwa bilionea Jeffrey Epstein akiwa ndani ya jela.

William Barr ameongeza kuwa, kifo cha Jeffrey Epstein kimezusha maswali magumu yanayopaswa kupatiwa majibu. 

Hadi sasa vyombo vya sheria vya Marekani havijathibitisha iwapo bilionea huyo rafiki mkubwa wa Trump alijinyonga au la, lakini maofisa wa serikali ya Marekani wanasema alijitia kitanzi yeye mwenyewe. 

Jeffrey Epstein alikutwa akining'inia katika jela ya Marekani wakati alipokuwa akisubiri kesi yake mahakamani kwa tuhuma za kufanya magendo ya watoto na wasichana wanaotumiwa katika utumwa wa ngono.

Warepublican wanakihusisha kifo cha bilionea huyo na rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ambaye wakati mmoja alikuwa mtu wa karibu sana kwa bilionea huyo. 

Rais Donald Trump pia ameandika katika ujumbe wa Twitter kwamba: Epstein alikuwa na taarifa zinazohusiana na Bill Clinton.  

Ufaransa pia imeitaka Marekani iiruhusu kufanya uchunguzi kuhusiana na harakati na shughuli za Jeffrey Epstein anayeandamwa na tuhuma za kufanya magendo ya watoto wadogo wanaotumiwa katika utumwa wa ngono.      

Tags