Jahangiri: Marekani inalenga kuvuruga usalama wa Ghuba ya Uajemi
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Eshaq Jahangiri amesema Marekani inalenga kuvuruga usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la kistratijia la Hormuz na kutumia ukosefu wa usalama kama kisingizo cha kujiimarisha kijeshi katika eneo.
Jahangiri ameyasema hayo Jumatatu alipokutana na Waziri Mkuu wa Russia Dmitri Medvedev katika mji wa Awaza nchini Turkmenistan pembizoni mwa mkutano wa kwanza wa Jukwaa la Kiuchumi la Bahari ya Kaspi.
Jahangiri amemfahamisha Medvedev kuwa ingawa Iran imekuwa ikijaribu kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz kwa karne kadhaa sasa, lakini katika siku za hivi karibuni Marekani imekuwa ikivuruga usalama wa eneo hilo ili kupata kisingizio cha kuunda muungano wa majeshi ya wanamaji.
Jahangiri amesema Iran inatazamia kuwa Russia kama mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itachukua hatua za kuitahadharisha Marekani kuhusu hatua zake hizo za kichochezi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Russia amesema nchi yake haijabadilisha msimamo wake wa kuunga mkono mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA). Aidha amesema msimamo wa Iran baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ni wa kimantiki na imara. Medvedev amesema msimamo wa Russia kuhusu JCPOA ni sawa na wa Iran huku akisisistiza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kinyume cha sheria.