Mazungumzo ya viongozi wa Ufaransa na Marekani kuhusu Iran na JCPOA
(last modified Sun, 25 Aug 2019 12:51:35 GMT )
Aug 25, 2019 12:51 UTC
  • Mazungumzo ya viongozi wa Ufaransa na Marekani kuhusu Iran na JCPOA

Mivutano iliyopo baina ya Marekani na nchi za Ulaya zilizomo katika kundi la 4+1 kuhusiana na jinsi ya kuamiliana na Iran na kadhia nzima ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA bado ni moja ya mivutano mikubwa ya pande hizo mbili. Katika wiki za hivi karibuni, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alifanya mazungumzo mbalimbali na marais wa Iran na Marekani na kuja na mapendekezo ya kupunguza wasiwasi uliopo.

Jana jioni Macron alifanya mazungumzo na rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu masuala hayo. Ikulu ya Elize ya Ufaransa ilitangaza kuwa, katika mazungumzo yake na Macron yaliyofanyika kabla ya kuanza kikao cha viongozi wa G7, Trump alimwambia rais huyo wa Ufaransa kwamba yeye hataki kupigana vita na Iran, bali anataka kufikia makubaliano tu na Tehran. Macron alitumia fursa hiyo kumueleza Trump mapendekezo yake kuhusu Iran ambapo kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Tehran itaruhusiwa kuuza mafuta yake kwa muda maalumu katika mkabala wa kuacha msimamo wake wa kupunguza wajibikaji wake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.  

JCPOA

 

Baadhi ya duru za habari nazo zimerusha hewani sehemu fulani ya mapendekezo hayo ya Ufaransa kuhusu Iran. Kwa mujibu wa duru hizo, Iran itaruhusiwa kuuza mafuta yake kwa muda maalumu, lakini kwa sharti iachane na msimamo wake wa kupunguza kiwango cha kuheshimu kwake makubaliano ya JCPOA, vile vile ipunguze ushawishi wake katika eneo la Magharibi mwa Asia na ikubali kuanza mazungumzo. Lakini Iran imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba haitokubali kufanya mazungumzo mengine yoyote kuhusu mapatano ya JCPOA kwani mazungumzo yalimalizika zamani, lililobakia ni kuheshimiwa tu vipengee vya makubaliano hayo hasa baada ya Marekani kuamua kujitoa bila sababu katika mapoatano hayo ya kimataifa. Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema juzi Ijumaa tarehe 23 Agosti baada ya kuonana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwamba, sisi tunaamini kuwa mapatano ya JCPOA si kitu cha kufanyiwa mazungumzo mengine. 

Uklweli ni kwamba madai ya Trump kwamba anapigania kufikia makubaliano na Tehran yanakinzana kikamilifu na siasa na vitendo vyake. Hivi sasa serikali ya Marekani inaendesha siasa za kuiwekea Iran vikwazo vikubwa mno na mashinikizo ambayo hayajawahi kutokea, lakini wakati huo huo Trump anadai kwamba eti anataka kufikia mapatano na Iran. Kwa kweli rais huyo mshari wa Marekani anayependa sana mizozo, anajaribu kupotosha walimwengu anapodai kuwa anataka kufikia makubaliano na Tehran. Ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikasema wazi kwamba, haiko tayari kufanya mazungumzo na serikali ya rais laghai Trump na inayachukulia madai ya rais huyo wa Marekani kuwa ni aina fulani tu ya kutaka kulitwisha taifa la Iran matakwa na hila zake za kiudanganyifu.

 

Suala jingine muhimu lililozungumwa katika mazungumzo ya marais wa Marekani na Ufaransa, ni madai yasiyo na msingi ya marais hao kwamba kuna ulazima wa kuizuia Iran eti isimiliki silaha za nyuklia. Rais wa Ufaransa alidai kuwa, nchi yake na Marekani zina malengo na shabaha moja kuhusu Iran. Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Macron aliwaambia waandishi wa habari kuwa: Shabaha ya pamoja ya Marekani na Ufaransa ni kwamba wasiruhusu Iran imiliki silaha za nyuklia. 

Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshasema mara chungu nzima kuwa, haina nia kabisa ya kumiliki silaha za nyuklia. Haina nia hiyo kabisa kwa sababu ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, kutengeneza na kumiliki silaha za maangamizi ya umati zikiwemo za nyuklia. Zaidi ya hayo ni kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) nao umethibitisha mara chungu nzima katika ripoti zake kuwa miradi ya nyuklia ya Iran ni ya amani kikamilifu na kwamba Tehran haijakwenda kinyume na ahadi zake za kutumia nishati hiyo muhimu kwa malengo ya kiraia tu. Hivyo matamshi ya Rais wa Ufaransa kwamba shabaha za nchi yake na Marekani ni moja kuhusiana na Iran yamezusha maswali mengi na kutufanya tuitilie shaka nia hasa ya Emmanuel Macron katika kile anachojaribu kujionesha kuwa ni mpatanishi baina ya Marekani na Iran. Hasa kwa kuzingatia kuwa hata ikulu ya Ufaransa imeonesha wazi kwamba rais wa nchi hiyo anavutika zaidi upande wa Marekani licha ya kuweko hitilafu za hapa na pale baina ya nchi hizo mbili. 

Tags