Mkuu wa zamani wa Shirika la CIA akosoa udhaifu wa Trump
Mkuu wa zamani wa Shirika la Kisasusi la Marekani (CIA), sambamba na kukosoa matamshi ya kupenda vita ya Rais Donald Trump wa Marekani, kufuatia shambulizi la ndege zisizo na rubani za Wayemen kwenye taasisi za mafuta za Saudia ARAMCO, amesema kuwa udhaifu wa kiuongozi wa rais huyo wa Marekani, umekuwa changamoto kimataifa.
John O. Brennan, ameyasema hayo leo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, ni suala lisilo na shaka kwamba mgogoro huo umechochewa na hatua ya Trump ya kujitoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kisha kutangaza vita vya kiuchumi dhidi ya Iran. John Brennan ameongeza kuwa, hivi sasa Marekani inakabiliwa na changamoto ya usalama wa kitaifa na kimataifa kutokana na udhaifu wa kiutawala wa Rais Donald Trump na kusisitiza kuwa ili kuikwamua nchi hiyo katika mgogoro huo kunahitajika radiamali ya kistratijia itakayoungwa mkono na vyama vyote.
Inafaa kuashiria kuwa, kufuatia shambulizi la harakati ya wananchi ya Answarullah ya Yemen kupitia ndege zisizo na rubani dhidi ya taasisi za kusafisha mafuta za Shirika la Mafuta la Sadia ARAMCO, Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Marekani imejiandaa kufanya shambulizi la kijeshi ingawa bado inasubiria taarifa ya Saudia kuhusu muhusika wa hujuma hiyo. Shambulizi la harakati ya Answarullah dhidi ya taasisi za mafuta za Saudia linatajwa kuwa kubwa zaidi tangu utawala wa Aal-Saud pamoja na washirika wake waanzishe mashambulizi nchini Yemen mwaka 2015 hadi sasa.