Mahakama yasimamisha sera ya Trump dhidi ya wahamiaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57026-mahakama_yasimamisha_sera_ya_trump_dhidi_ya_wahamiaji
Jaji wa Mahakama ya Federali ya Wilaya ya Portland, jimboni Oregon ncini Marekani amesitisha kwa muda utekelezaji wa sera iliyotangazwa na utawala wa Rais Donald Trump ya kuwataka wahamiaji kuthibitisha kuwa wana uwezo wa kugharamia bima ya afya au matibabu kabla ya kupatiwa kibali cha kuingia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 03, 2019 08:04 UTC
  • Mahakama yasimamisha sera ya Trump dhidi ya wahamiaji

Jaji wa Mahakama ya Federali ya Wilaya ya Portland, jimboni Oregon ncini Marekani amesitisha kwa muda utekelezaji wa sera iliyotangazwa na utawala wa Rais Donald Trump ya kuwataka wahamiaji kuthibitisha kuwa wana uwezo wa kugharamia bima ya afya au matibabu kabla ya kupatiwa kibali cha kuingia nchini humo.

Katika kikao cha jana Jumamosi, Jaji Michael Simon alitangaza kuzuia kwa muda utekelezwaji wa kanuni hiyo ambayo ni jaribio la karibuni kabisa la utawala wa Trump la kuzuia wimbi la wahamiaji.

Raia saba wa Marekani na shirika lisilo la kiserikali walifungua faili la shauri hilo siku ya Jumatano, wakisisitiza kuwa sheria hiyo itazuia karibu theluthi mbili ya wahamiaji halali kuingia Marekani.

Shauri hilo lilisema pia kanuni hiyo itapunguza au kuondoa kwa sehemu kubwa idadi ya wahamiaji wanaoingia Marekani chini ya utaratibu wa vibali vinavyodhaminiwa na familia zao.

Polisi ya Marekani ikiwatenganisha wazazi na watoto katika mpaka wa Mexico

Siasa hizo za kuwapinga wahajiri za Rais Donald Trump wa Marekani zimepingwa vikali katika miezi ya hivi karibuni na mataifa na taasisi mbalimbali za dunia. 

Novemba mwaka 2016 na hata kabla ya kuapishwa, Trump aliahidi kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, likiwemo suala la kuwatimua wahamiaji milioni 3 nchini humo.