Waziri Mkuu wa Malaysia: Huwenda Marekani ikatuma droni na kunitungua
Mahathir Mohamad Waziri Mkuu wa Malaysia ameikosoa na kuilaani vikali Marekani kwa kumuuwa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na kwa kutekeleza mauaji wakati wowote.
Akizungumza mbele ya waandishi habari jana Jumanne, Mahathir Muhammad alisema kuwa shambulio lililofanywa na droni za Marekani dhidi ya Kamanda Soleimani ni kinyume na sheria za kimataifa.
Waziri Mkuu wa Malaysia amezitolea wito nchi za Kiislamu kuungana ili kujilinda zenyewe dhidi ya vitisho vya nchi ajinabi. Amesema ni wakati mwafaka sasa kwa nchi za Kiislamu kuungana na kuwa kitu kimoja.
Mahathir Mohamad amesema nchi za Kiislamu haziko salama tena.
Alfajiri Ijumaa iliyopita ndege isiyo na rubani ya Marekani ilishambulia karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na kumuuwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandes aliyekuwa Naibu Mkuu wa Harakati ya Wapiganaji wa Kujitolea wa Iraq (al Hashd al Shaabi) na wenzao wanane.

Kufuatia mauaji hayo ya kigaidi, Iran imeahidi kulipiza kisasi kwa Marekani.