Feb 08, 2020 07:32 UTC
  • Ombi la Rais wa Ufaransa la kuangamizwa silaha za nyuklia

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, jana Ijumaa alitangaza uamuzi wa nchi yake wa kupunguza idadi ya silaha zake za nyuklia hadi chini ya vichwa 300 vya nyuklia.

Macron alionya kuwa, nchi za Ulaya haziwezi kuwa watazamaji tu katika mashindano ya silaha za nyuklia. Amezitaka nchi za Ulaya kuanzisha mchakato wa kimataifa wa kudhibiti silaha za nyuklia.

Rais wa Ufaransa amesema uamuzi wa nchi yake wa kupunguza silaha zake za nyuklia unalenga kuhalalisha ombi la nchi hiyo la kutaka madola mengine yenye silaha za nyuklia kupunguza silaha hizo hatari kote duniani.

Hayo yanajiri wakati ambao, Rais Donald Trump wa Ufaransa anatekeleza mkakati wa kuiondoa nchi yake katika mikataba muhimu ya kimataifa ya kudhibiti silaha za nyuklia ili nchi hiyo iwe na uhuru zaidi wa kuimarisha uwezo wake wa silaha hizo za maangamizi ya umati. Baada ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Wastani INF, mnamo Agosti 2 2019, utawala wa Trump ulitangaza kuanzisha mchakato  wa kujiondoa katika mkataba muhimu sana wa silaha unaojulikana kama New START ambao ni baina ya Russia na Marekani kuhusu kupunguzwa silha za kistratijia za nyuklia.

Mpango huo wa Marekani umewaweka wasiwasi mkubwa waitifaki wake barani Ulaya; hasa nchi kama vile Ufaransa ambayo imeanzisha mchakato wa kupunguza silaha zake za nyuklia.

Silaha za nyuklia

Wasi wasi wa Macron unatokana na hali ya hivi sasa ya kusambaratika mikataba muhimu ya kimataifa inayohusu udhibiti au upunguzaji wa silaha za nyuklia. Nchi za Ulaya zina hofu kubwa hasa baada ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa INF na baada ya hapo pia ikakataa kujadidisha mkataba  wa New START, na hivyo Russia nayo, kama nchi yenye uwezo mkubwa wa silaha za nyuklia ambayo ni mshindani mkuu wa Marekani, ikachukua hatua kama hiyo.

Dan Smith, Mkurugenzi wa Shirika la Stockholm la Utafiti wa Amani ya Kimataifa (SIPRI) katika kujibu swali kuhusu matokeo muhimu zaidi kuhusu Marekani na Russia kuacha kutekeleza mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Wastani alisema: "Kwa mtazamo wangu kadhia hii ya udhibiti wa silaha za nyuklia imekumbwa na mgogoro mkubwa.

Kufutwa mkataba wa INF kumesababisha wasi wasi kwani kutaanza kushuhudiwa tena mashindano makubwa ya silaha baina ya Marekani na Russia barani Ulaya. Rais Vladimir Putin wa Russia ameashiria hatua ya Marekani kujiondoa katika INF na kusema: "Hatua hii ya Marekani imepelekea kuwa mbaya hali jumla ya usalama barani Ulaya."

Baada ya kufutwa rasmi INF baina ya Marekani na Russia, wakuu wa Ulaya walitahadharisha kuhusu mashindano mapya ya silaha baina ya nchi mbali mbali na kutangaza kuwa, bara Ulaya litadhurika na matokeo hasi ya kufutwa mkataba huu unaohusu makombora. 

Jenerali Ebenhard Zorn, Mkaguzi Mkuu wa Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, amebainisha wasi wasi wake kuhusu kuftwa INF na ametaka kutayarishwe mkataba mpya katika uga huo. Jenerali Zorn anafafanua zaidi kwa kusema: "Kwa mtazamo wangu, kuna haja ya kuanzisha mfumo mpya wa kudhibiti silaha baina ya nchi za dunia...mapatano haya mapya yanapaswa kuwa kigezo cha kudhabiti usalama wa Ulaya na Ujerumani."

Hivi sasa, utawala wa Trump unatekeleza mkakati wa kuhakikisha kuwa hautii saini upya mkataba wa New Start wa kuweka vizingiti katika silaha za kistratijia za nyuklia za Russia na Marekani. Lengo la Marekani la kutaka mkataba huo usijadidishwe ni kuiwezesha kuimarisha silaha zake za nyuklia. Katika upande wa pili Russia kwa mara kadhaa sasa imetaka kuanzishwe mazungumzo kwa lengo la kutia saini upya mkataba huo muhimu sana wa kudhibiti au kupunguza silaha za nyuklia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov mwezi Disemba mwaka 2019 alitaka kutiwe saini upya mkataba wa New Start bila masharti au vizingiti vyovyote. Rais Vladimir Putin wa Russia naye amesema nchi yake iko tayari kutia saini upya mkataba huo wakati wowote ule. Kutangazwa kuwa tayari Russia kufanya mazungumzo kuhusu udhibiti wa silaha kunaweka wazi visingizio vya Marekani vya kukwepa mazunguzo katika uga huo.

Mkataba wa INF

Kutotiwa upya saini mkataba wa New START kutokana na vizingiti vilivyowekwa na Marekani kutapelekea kuongezeka ukosefu wa usalama katika uga wa kimataifa na kuongezeka kasi ya mashindano ya silaha za nyuklia baina ya madola makubwa yenye uwezo wa silaha za nyuklia duniani. Kati ya malengo ambayo Marekani inayafuatilia katika kadhia hii ni kuilazimisha Russia kuingia katika mashindano mpya ya silaha na kwa msingi huo kudhoofisha zaidi uchumi wa nchi hiyo kwani italazimika kuwekeza zaidi katika masuala ya kijeshi.

Tags