Uamuzi wa Marekani wa kushadidisha vikwazo vya mafuta dhidi ya Venezuela
(last modified Wed, 26 Feb 2020 13:06:50 GMT )
Feb 26, 2020 13:06 UTC
  • Uamuzi wa Marekani wa kushadidisha vikwazo vya mafuta dhidi ya Venezuela

Serikali ya Marekani ikiwa na lengo la kuendeleza mashinikizo dhidi ya Venezuela imeazimia kushadidisha vikwazo vya mafuta dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Elliott Abrams, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Venezuela amesema kuwa, Rais Donald Trump amechukua uamuzi wa kushadidisha vikwazo vya mafuta dhidi ya Venezuela na kwamba, watu na mashirika ambayo yatakiuka vikwazo hivyo yatachukuliwa hatua kali.

Kuanzia mwaka 2019 Marekani ikiwa na lengo la kuipundua serikali ya Rais Nicolas Maduro iliiwekea vikwazo mbalimbali serikali ya mrengo wa kushoto ya nchi hiyo ambayo inapinga ubeberu. Vikwazo hivyo vilijumuisha sekta ya nishati na mafuta pia.

Kwa mujibu wa vikwazo hivyo, serikali ya Marekani ilipiga marufuku kununuliwa mafuta ya Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela. Aidha endapo mataifa na mashirika ya kigeni yatatumia mfumo wa kibenki wa Marekani kwa ajili ya mabadilishano yao ya kifedha katika biashara ya mafuta, nayo yatakabiliwa na faini na vikwazo vya serikali ya Washington.

Kwa muda sasa viongozi wa Marekani wameiwekea Venezuela vikwazo tofauti tofauti katika sekta ya uchumi hususan nishati, biashara na mfumo wa benki lengo lao hasa likiwa ni kushadidisha matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo na kibadilisha anga ya ndani iwe kwa maslahi ya wapinzani wanaoungwa mkono na serikali ya Washington.

Hatua ya viongozi wa Marekani ya kuiwekea vikwazo Venezuela hususan katika sekta ya mafuta inalenga kusitisha usafirishwaji nje ya nchi mafuta ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini na kwa msingi huo kuzidi kuzorotesha uchumi wa nchi hiyo.

Fernandez Pascualio, Katibu Mkuu wa Baraza la Ulinzi la Venezuela anasema kuwa, daima Marekani imekuwa na jicho la tamaa kwa mali na utajiri wa Venezuela na ndio maana imeanzisha vita vya pande kadhaa dhidi ya nchi hiyo.  Aidha anasema: Marekani imekuwa ikifanya mambo kama utawala ambao unataka kumiliki kila kitu cha Venezuela na hii ndio sababu na chimbuko la hitilafu zote.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Hata hivyo hadi sasa njama za Marekani hazijazaa matunda kwani Rais Maduro akipata himaya na uungaji mkono wa wananchi na jeshi amefanikiwa kurejesha utulivu nchini Venezuela na hata kutatua baadhi ya matatizo ya kiuchumi akishirikiana na waitifaki wake. Rais Maduro amefanikiwa hasa katika uga wa nishati ya mafuta kuyashinda matatizo na changamoto zilizotokana na vikwazo vya Marekani.

Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela limetangaza kuwa, licha ya mashiinikizo yote ya Marekani, lakini shughuli za uzalishaji mafuta zinaendelea kama kawaida na shirika hilo limefanikiwa kuvishinda vikwazo. Shughuli kuu na muhimu zinaendelea kama kawaida katika taasisi za mafuta za nchi hiyo.

Hali hii ya kushindwa na kugonga mwamba Marekani katika kuikwamisha sekta ya mafuta ya Venezuela ni jambo ambalo limeifanya serikali ya Trump ishadidishe mashinikizo na vikwazo vya mafuta dhidi ya Venezuela. Ni kwa muktadha huo, ndio maana serikali ya Marekani imetangaza kuwa, wanunuzi wa mafuta ya Venezuela wakiwemo kutoka Asia na hata wanaoisadia serikali ya Caracas ikwepe vikwazo watafuatiliwa popote walipo na kuwekewa vikwazo.

Rais Donald Trump wa Marekani

Imepangwa kuwa katika majuma na miezi ijayo, Marekani itawaonya watu na mashirika ambayo yanahusika katika sekta ya mafuta ya Venezuela na hatua itakayofuata ni kuwekewa vikwazo zaidi.

Licha ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela kutofanikiwa, lakini viongozi wa Washington wangali wanang'ang'ania kuendeleza vikwazo hivyo na kujaribu kubana duara la vikwazo hivyo dhidi ya nchi hiyo, mashirika na nchi ambazo zina mabadilishano ya kifedha na mafuta na Venezuela.

Pamoja na hayo inaonekana kuwa, kung'anng'ania hilo pia na mashinikizo ya Marekani dhidi ya washirika wa Venezuela ni jambo ambalo nalo halitaifanya Washington ifikie malengo yake ambayo ni kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nicolas Maduro na kuiweka madarakkni serikali ambayo itakuwa ni kibaraka wake.

Akiashiria kushindwa njama za Marekani za kushadidisha mzingiro wav kiuchumi dhidi ya Venezuela, Rais Nicolas Maduro amesema kuwa, Washington haifahamu na kudiriki nguvu ya wananchi.

Tags