Jun 15, 2020 14:59 UTC
  • Erdogan: Uchumi wa Kiislamu unaweza kuiondoa dunia katika mgogoro

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema uchumi wa Kiislamu ndiyo dawa mjarabu ya kuiondoa dunia katika mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na janga la corona.

Erdogan alisema hayo jana Jumapili na kufafanua kuwa, "mfumo wa uchumi wa Kiislamu ndio ufunguo wa kuunusuru uchumi wa dunia unaoendelea kuvurugwa na janga la corona."

Rais wa Uturuki amesema hayo katika duru ya 12 la Kongamano la Kimataifa la Uchumi na Fedha la Kiislamu ambapo pia amesema nchi yake inapania kuufanya mji wa Istanbul kuwa kitovu cha uchumi wa Kiislamu.

Amebainisha kuwa, "kinyume kabisa na yale yaliyoahidiwa, usambazaji wa mapato na utajiri unazidi kuharibika kote duniani, huku mwanya baina ya nchi na nchi ukizidi kupanuka."

Mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu unawajali matajiri na maskini

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameeleza bayana kuwa, kupoteza maisha watu 440,000 kwa corona hakuwezi kuhusishwa tu na ugonjwa huo, lakini kumetokana pia na mifumo mibaya ya uchumi katika nchi mbali mbali duniani, ambayo inalinda tu matajiri na wenye nguvu.

Amesema, "katika baadhi ya nchi, watu ambao hawakuwa na bima ya afya waliachwa wafe. Hata nchi zilizostawi kiuchumi zilishindwa kuwapa wananchi wao barakoa na huduma za afya za kiwango cha chini." 

 

 

Tags