Jun 16, 2020 08:03 UTC
  • Waziri Zarif aelekea Russia baada ya kuitembelea Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameelekea Moscow, mji mkuu wa Russia katika ziara rasmi ya kikazi baada ya kuitembelea Uturuki na kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Mohammad Javad Zarif ameenda Moscow baada ya kusema kuwa amefanya mazungumzo ya kufana na viongozi wa ngazi za juu wa Uturuki katika mji wa Istanbul.

Amekutana na mwenzake wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo, ambapo wamezungumza kuhusu uhusiano wa pande mbili, na masuala ya kieneo na kimataifa.

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Dakta Zarif amesema: Tumebadilishana mawazo na kufanya mazungumzo ya kina kuhusu ushirikiano wa pande mbili, na pia masuala ya kieneo na kimataifa. Mazungumzo yetu yamefana. Kituo kijacho, Moscow. Majirani daima ni kipaumbele chetu.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uturuki mjini Istanbul

Akiwa mjini Istanbul hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kuwa, "kuimarisha uhusiano na majirani zetu katika eneo ni katika vipaumbele vya sera za kigeni za Iran."

Dakta Zarif aliitembelea Syria mnamo Aprili 20 licha ya janga la corona na kusisitiza kuwa, Iran inalipa uzito suala la kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na nchi za eneo na majirani zake.

 

Tags