Watu 140 wafariki dunia kwa mafuriko China
(last modified Wed, 15 Jul 2020 07:40:45 GMT )
Jul 15, 2020 07:40 UTC
  • Watu 140 wafariki dunia kwa mafuriko China

Serikali ya China imetangaza kuwa watu takriban 140 wameaga dunia baada ya nchi hiyo kuathiriwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kuikumba China katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 nchini humo. Aidha watu milioni 38 wameathiriwa na mafuriko hayo na nyumba elfu 28 zimebomoka.

Wizara ya Maji ya China imetangaza kuwa, mito 33 imefurika huku tahadhari ikitolewa kuhusu jumla ya mito 433. Majimbo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Jiangxi, Hubei, Hunan, Anhui, Zhejiang, Jiangsu na Chongqing.

Rais Xi Jinping amezitaka mamlaka husika kwenye maeneo yaliyoathirika kuchukua hatua zaidi ili kuwasaidia wananchi walioathirika na janga hilo. Mvua zimekuwa zikinyesha katika baadhi ya maeneo nchini Chino tangu mwezi uliopita.

Wizara inayoshughulikia majanga ya China Ijumaa iliyopita ilitangaza kuwa watu 141 wameaga dunia au kutoweka na hasara ya kiuchumi inakadiriwa kuwa ya Yuan bilioni 60 sawa na dola za Kimarekani bilioni 8.57.

Wakati huo huo Mamlaka ya Hali ya Hewa ya China imetupilia mbali wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokea mafuriko makubwa zaidi nchini humo kama yale yaliyoshuhudiwa mwaka 1998.