UN, Uturuki zakosoa hukumu ya Saudia dhidi ya wauaji wa Khashoggi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63293-un_uturuki_zakosoa_hukumu_ya_saudia_dhidi_ya_wauaji_wa_khashoggi
Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa amekosoa vikali hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Saudi Arabia dhidi wahusika wa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa Saudia aliyeuliwa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018.
(last modified 2026-04-24T06:29:55+00:00 )
Sep 08, 2020 03:23 UTC
  • UN, Uturuki zakosoa hukumu ya Saudia dhidi ya wauaji wa Khashoggi

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa amekosoa vikali hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Saudi Arabia dhidi wahusika wa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa Saudia aliyeuliwa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018.

Agnes Callamard, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mauaji ya kiholela amekosoa vikali hukumu hiyo iliyowavua adhabu ya kifo wahusika wa mauaji hayo. Amesema hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya Saudia baada ya kumalizika mchakato wa kesi ambazo hazikuwa na uwazi, usawa wala uadilifu.

Ripota huyo maalumu wa UN katika masuala ya mauaji ya kiholela amesema kutolewa hukumu hiyo ni sawa na kuudhihaki mfumo wa sheria. Vyombo vya habari vya Saudia vimetangaza kuwa, watuhumiwa watano wa mauaji hayo wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, huku wengine watatu wakihukumiwa vifungo vya kati ya miaka 7 hadi 10 jela.

Wakati huohuo, Uturuki imesema hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Saudia ni kinyume kabisa na matarajio ya serikali ya Ankara. Fahrettin Altun, Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Ofisi ya Rais wa Uturuki ameutaka utawala wa Riyadh kushirikiana na Ankara katika kuchunguza faili jeusi la mauaji hayo ya kikatili.

Mchumba wa Jamal Khashoggi, Khadija Genghis amekosoa vikali hukumu hiyo ya Saudia

Ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Hadi sasa hatujui nini kilichofanyika kwa mwili wa Kashoggi, ni nani aliyetaka auawe, na je ni nani washirika wa mauaji hayo hapa nchini. Tunautilia shaka uhalali wa mchakato wa kesi hizo."   

Hii ni katika hali ambayo, mwezi Machi mwaka huu, waendesha mashtaka wa Uturuki waliwafungulia mashtaka bila wenyewe kuwepo mahakamani raia 20 wa Saudi Arabia kwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi, wakiwemo wasaidizi waandamizi wawili wa zamani wa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman.