Sep 18, 2020 08:06 UTC
  • Russia: Amani haitapatikana Asia Magharibi bila kutatuliwa kadhia ya Palestina

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema ni kosa kudhani kuwa amani ya kudumu itapatikana katika eneo la Asia Magharibi pasi na kutatuliwa mgogoro wa Palestina.

Katika taarifa, wizara hiyo imeashiria kuhusu hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, amani ya kudumu Asia Magharibi itapatikana tu iwapo suala la Palestina litapatiwa ufumbuzi.

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, ni muhali kupatikana uthabiti katika eneo iwapo matatizo ya Wapalestina yataendelea kupuuzwa sambamba na kuendelea kuporwa ardhi zao kwa ajili ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia kadhalika imetoa mwito wa kuweko jitihada za pamoja za kimataifa kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Palestina. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: "Tunatoa mwito kwa washiriki wetu wa kieneo na kimataifa kuongezea jitihada za pamoja katika suala hili muhimu."

Maandamano ya kulaani usaliti wa Imarati na Bahrain; na kuwapa mgongo Wapalestina

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeongeza kuwa, "Moscow iko tayari kwa ushirikiano huu utakaojumusha fremu ya Kamati ya Pande Nne ya kutatua mzozo wa Mashariki ya Kati, inayozijumuisha Marekani, Russia, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na kwa ushirikiano wa karibu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu."

Viongozi wa kisiasa na kidini wa Palestina na eneo la Asia Magharibi wamesisitiza kuwa, kanda hii haitashuhudia amani hadi pale utawala ghasibu wa Israel utakapoacha kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Tags