Serikali ya Myanmar na hali mbaya ya Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i6358-serikali_ya_myanmar_na_hali_mbaya_ya_waislamu_wa_rohingya
Katika hali ambayo matatizo ya Waislamu wa Rohingya katika kambi za wakimbizi yanaendelea kushuhudiwa, makundi yanayofungamana na Waislamu yametoa ripoti kuhusiana na matatizo mapya yanayowakabili Waislamu hao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 04, 2016 07:53 UTC
  • Serikali ya Myanmar na hali mbaya ya Waislamu wa Rohingya

Katika hali ambayo matatizo ya Waislamu wa Rohingya katika kambi za wakimbizi yanaendelea kushuhudiwa, makundi yanayofungamana na Waislamu yametoa ripoti kuhusiana na matatizo mapya yanayowakabili Waislamu hao.

Makundi yanayofungamana na Waislamu wa Rohingya yamefichua kwamba, mbali na kukabiliwa na jinai za chuki dhidi ya Uislamu za vikosi vya serikali ya Myanmar na makundi yenye misimamo mikali ya Mabudha, Waislamu hao filihali wanakumbwa na matatizo mengi kama uhaba wa maji safi ya kunywa, kuzuka maradhi, kutopata huduma za tiba na afya na kutokuweko mashirika ya utoaji misaada ya kibinaadamu katika maeneo hayo.

Mmoja wa wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wa Rohingya amesema kuwa, serikali ya Myanmar inatumia silaha ya huduma ya afya kwa ajili ya kuwaangamiza Waislamu.

Mwanaharakati huyo ametoa ripoti na kuonesha picha na kusisitiza kwamba, Waislamu na wafuasi wa dini za walio wachache wanataabika kutokana na mateso na kunyimwa huduma za afya. Takwimu zinaonesha kuwa, hali ya huduma za afya ni mbaya baina ya Waislamu hao huku kukiripotiwa kuibuka maradhi. Hali ikiwa ni hivyo, serikali ya Myanmar inazuia hatua zozote zile za kutaka kufikishiwa huduma za afya Waislamu hao. Aidha ikiwa ni katika kuzidi kuwashinikiza zaidi Waislamu wa Rohingya, hivi karibuni mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wakishirikiana na vyombo vya usalama walifunga misikiti ya jimbo la Rakhine.

Mabudha hao walitaka kujenga mahekalu mahala pa misikiti hiyo, hatua ambayo ilikabiliwa na onyo kali kutoka kwa Waislamu hao na jamii ya kimataifa.

Kwa sasa Mabudha hao wakiwa na lengo la kuwatesa kiroho Waislamu wameweka masanamu mbele ya misikiti hiyo. Katibu Mkuu wa Masuala ya Dini ya Kiislamu nchini Myanmar ametoa indhari juu ya matokeo mabaya ya kuwekwa masanamu ya mabudha jirani na misikiti kusini mwa nchi hiyo na kusisitiza kwamba, hatua hiyo itapelekea kutokea mapiganao katika eneo hilo. Kiongozi huyo wa Kiislamu amewataka wakazi wa eneo hilo kutumia njia ya mazungumzo katika kuzuia uwekwaji wa masanamu ya mabudha mbele ya misikiti. Hivi karibuni pia kundi la viongozi wa Mabudha liliweka sanamu jirani na msikiti mkuu kusini mwa nchi hiyo.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, vitendo hivyo vinafanyika ili kuwachochea Waislamu hao wa Rohingya.

Kuna takribani Waislamu milioni moja wa Rohingya wanaoisha katika kambi kwenye mji wa Rakhine na viongozi wa nchi hiyo wanawatambua Waislamu hao kama wahamiaji haramu kutoka Bangladesh. Ripoti zinaonesha kuwa, kwa sasa Waislamu hao wanaishi katika mazingira magumu mno.

Kuuawa makumi ya Waislamu wa Rohingya kumeiweka serikali mpya ya nchi hiyo katika mazingira magumu ya kutoa majibu kwa fikra za waliowengi ulimwenguni kuhusiana na hali ya Waislamu hao.

Siku chache zilizopita boti iliyokuwa imewabeba Waislamu wa Rohingya ilizama na kuuwa zaidi ya watu 30.

Pamoja na hali hiyo mbaya inayowakabili Waislamu wa Rohingya, Aung San Suu Kyi kiongozi wa chama tawala cha nchi hiyo cha National League for Democracy ameendelea kunyamaza kimya na kutozungumzia hali hiyo.

Waislamu wa Rohingya walianza kuandamwa na mashambulio ya mabudha wenye misimamo mikali kuanzia mwaka 2012 katika mkoa wa Rakhine na zaidi ya elfu moja kati yao wameuawa kinyama, huku zaidi ya laki moja wakilazimika kuyakimbia makazi yao.

Hivi sasa ripoti zinazotolewa zinaonesha kuwa, Waislamu hao wanaishi katika mazingira mabaya kabisa kwenye kambi hizo ndani ya Myanmar na katika jirani, jambo ambalo linailazimu jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya kushughulikia matatizo ya Waislamu hao na kuboresha hali zao.