Tishio la Mike Pompeo la kufunga ubalozi wa Marekani mjini Baghdad
Marekani imekuwa nchini Iraq kwa upana zaidi tangu mwaka 2014 kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na hadi sasa kuna maelfu ya wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Hatua zisizo za kisheria za Marekani zimekuwa sababu ya kuibuka na upinzani mkali dhidi ya uwepo wa Washington nchini Iraq sambamba na kuongezeka hujuma na mashambulio dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.
Katika radiamali yake kwa jambo hilo, serikali ya Trump imetishia kuwa, itafunga ubalozi ulioko mjini Baghdad. Gazeti la New York Times limewanukuu maafisa watatu wa Marekani na kuandika: Mike Pompeo amesema kuwa, endapo hujuma na mashambulio hayo hayatazuiwa, basi ubalozi wa Marekani mjini Baghdad utafungwa na inawezekana uamuzi huo ukatekelezwa hata kabla ya kufanyika uchaguzi nchini Marekani Novemba mwaka huu. Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, endapo mpango wa kufungwa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad utatekelezwa, Matthew Tueller balozi wa nchi hiyo nchini Iraq atahamishiwa katika ubalozi mdogo wa Erbil au katika kambi ya kijeshi ya Washington ya Ain al-Assad.

Kuuawa kigaidi na kinyume cha sheria, Luteni Jenerali Qassim Suleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al-Mohandes Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashd al-Shaabi ya Iraq pamoja na watu waliokuwa wameandamana nao katika Uwanja wa Ndege wa Baghdad Januari mwaka huu jinai iliyofanywa na Marekani, kulipelekea kuibuka wimbi kubwa malalamikko na kilichofuata ni mashambulio na hujuma dhidi ya kambi za Marekani na ubalozi wa nchi hiyo huko Baghdad.
Katika miezi ya karibuni, ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, misafara ya kijeshi na vituo vya askari wa jeshi la kigaidi la nchi hiyo vilivyoko nchini humo vimeandamwa na mashambulio kadhaa ambayo yamechukua mkondo wa kuongezeka.
Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba, kinyume na madai ya Marekani kwamba, inadhibiti hali ya mambo nchini Iraq na hata imechukua hatua ya kuweka mfumo wa makombora wa Patriot katika ubalozi wake mjini Baghdad, lakini bado Washington inakabiliwa na wasiwasi mkubwa na ndio maana inafikiria kufunga ubalozi wake huo na kuuhamishia sehemu nyingine. Pompeo amedai kuwa, hataki kushuhudia hujuma na shambulio jingine dhidi ya ubalozi wa Marekani kama lile la mwaka 2012 mjini Benghazi Libya ambapo wanadiplomasia wake wanne waliuawa.

Licha ya hali hii, lakini msimamo wa serikali ya Trump kuhusiana na hili bado haueleweki. Marekani imewatangazia waitifaki wake kwamba, uamuzi wa kufunga ubalozi huo mjini Baghdad umeshachukuliwa.
Hata hivyo kabla ya kufunga ubalozi huo, Marekani itachukua hatua ya kutathmini tena uamuzi wake huo. Fadhil Abu Raghif, mweledi na mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Iraq anasema: Suala la kufungwa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad si jambo la kutekelezwa kikweli kweli, kwani utekelezaji wake maana yake ni kushindwa haiba ya kijeshi ya Marekani.
Samuel Werberg, msemaji wa kieneo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alisisitiza Jumanne ya juzi kwamba, ubalozi wa nchi hiyo mjini Baghdad, licha ya kukabiliwa na changamoto zilizopo, utaendelea na shughuli zake na kwa sasa hautafungwa.
Pamoja na madai hayo, lakini kushadidi hujuma na mashambulio dhidi ya Wamarekani nchini Iraq, kumeufanya uwepo wao wa kijeshi katika nchi hiyo ukabiliwe na changamoto kubwa. Hasa kwa kuzingatia kwamba, kimsingi utendaji wa Washington mkabala na Iraq ni kama kikosi vamizi kilichoikalia kwa mabavu nchi fulani.

Viongozi wa Marekani wamekuwa hawaoni kama wana jukumu la kuwajulisha viongozi wa Iraq au kufanya uratibu nao kuhusiana na hatua zake kama lilivyo suala tarajiwa la kufungwa ubaliozi wa Marekani mjini Baghdad, bali wamekuwa wakifanya mambo yao watakavyo.
Hatua ya Marekani ya kuipuuza kikamilifu serikali ya Iraq imeshuhudiwa mara chungu nzima ambapo Washington imekuwa ikifanya mashambulio dhidi ya kambi za Harakati ya Wananchi ya Hashd al-Shaabi bila ya kuwajulisha viongozi wa Baghdad.
Mashambulio hayo yamekuwa yakifanywa kwa kisingizio cha kujibu hujuma na mashambulio dhidi ya kambi zake au dhidi ya ubalozi wake. Ukweli wa mambo ni kuwa, muamala na utendaji wa Marekani nchini Iraq hauna tofauti kabisa na utendaji wa dola vamizi, kwani Washington imeendelea kukiukka waziwazi mamlaka ya kitaifa ya kujitawala nchi hiyo.