Oct 18, 2020 04:24 UTC
  • China yaruhusu matumizi ya chanjo ya COVID-19 ya CoronaVac

Mji wa Jiaxing ulioko mashariki mwa China jana uliidhinisha matumizi ya chanjo ya virusi vya corona ya CoronaVac ambayo imeingizwa sokoni na kuanza kuuzwa kwa gharama ya dola 60 za kimarekani.

Mamlaka ya mji wa Jianxing ilianza kutoa chanjo hiyo ya majaribio jana Jumamosi kwa wafanyakazi na wahudumu wanaokabiliwa zaidi ya hatari ya virusi vya corona.

Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Maradhi ya China imesema kuwa chanjo hiyo inatolewa katika dozi mbili na kwamba tayari imeanza kutolewa kwa wafanyakazi wa sekta muhimu wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya tiba.

Chanjo ya COVID-19 ya  CoronaVac ilikuwa tayari imeanza kufanyiwa majaribio kwa mamia ya maelfu ya watu na kuingia awamu yake mwisho ya majaribio hayo yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu.

Majaribi ya chanjo hiyo yaliingia awamu yake ya mwisho katika nchi za Brazil, Indonesia na Uturuki.

China imeanza kutumia chanjo ya CoronaVac

Kampuni ya Sinovac iliyotengeneza chanjo hiyo imesema kuwa taarifa kamili kuhusiana na awamu ya tatu na ya mwisho ya chanjo ya CoronaVac itatolewa mapema mwezi ujao wa Novemba.

Wakati huo huo nchi nyingi duniani zimeendelea kuchukua hatua kali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vimeshadidi tena katika maeneo mbalimbali ya dunia.  

Zaidi ya watu 1,111,807 wameaga dunia kote duniani kutokana na virusi vya corona na 39,777,221 walikuwa wameambukizwa virusi hivyo hadi jana Jumamosi. 

Tags