Iran, China na Russia zazitaka nchi za Magharibi zianze tena kutekeleza makubaliano ya nyuklia
Iran, China na Russia zimesisitiza kuwa, vifungu vya mkataba wa nyuklia wa JCPOA vingali vina itibari na kuzishauri nchi za Magharibi ambazo zimekwamisha utekelezaji wa mapatano hayo kwa kutochukua hatua na kukhalifu kutekeleza ahadi na majukumu yao, zionyeshe utashi wa kisiasa na kuchukua hatua zinazohitajika ili kuanza kutekeleza tena makubaliano hayo.
Iran, China na Russia zimesisitiza kuwa, kwa muda wote huo hazijaacha kufanya kila juhudi ili kuyarejesha makubaliano ya JCPOA na kukumbusha kuwa kutokana na matokeo yaliyopatikana kwenye duru nane za mazungumzo ya Vienna, zinatangaza utayarifu wao wa kufikia tena makubaliano ya kuanza kutekeleza JCPOA kulingana na matini ya Agosti 2022.
Mazungumzo ya kuanza kutekeleza tena JCPOA yalifanyika kuanzia tarehe 27 Disemba 2021 mjini Vienna katika duru nane kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Kundi la 4+1, Umoja wa Ulaya na Iran.
Ujumbe wa Marekani nao pia ulishiriki kwenye mazungumzo hayo kwa njia isiyo ya moja kwa moja, lakini mazungumzo hayo yaliishia kwenye mkwamo kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na migongano katika muamala, kuchelewa kuchukua uamuzi, kujivutia zaidi maslahi yake Marekani na kuibua matakwa mengine mapya.../