May 26, 2024 11:15 UTC
  • NATO yaituhumu China kuwa inachochea moto wa vita Ulaya kwa kuiunga mkono Russia

Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la Magharibi NATO Jens Stoltenberg ameituhumu China kwamba inachochea vita barani Ulaya kwa kuiunga mkono Russia dhidi ya Ukraine.

Stoltenberg ametoa tuhuma hizo katika mahojiano na gazeti la Ujerumani, la Welt am Sonntag kwa kusema: "China inasema inataka kudumisha uhusiano mzuri na nchi za Magharibi. Hata hivyo, wakati huo huo, Beijing inachochea vita barani Ulaya. Huwezi kuwa na njia zote mbili" .

Stoltenberg ametilia mkazo kile alichokielezea kuwa mchango muhimu wa China kwa kuiunga mkono Russia katika mzozo wa Ukraine.

Katibu Mkuu wa NATO amebainisha kuwa kuna ongezeko la waziwazi la uuzaji vipuri vya mashine, vifaa vidogo vya elektroniki na teknolojia nyingine ambazo Moscow inazitumia kuundia makombora, vifaru na ndege katika vita dhidi ya Ukraine.

Rais Vladimir Putin wa Russia (kushoto) na Rais Joe Biden wa Marekani

Stoltenberg amerudia kueleza kwamba hakuna mpango wa kupelekewa wanajeshi wa NATO nchini Ukraine au kupanua mwavuli wa ulinzi wa anga wa muungano huo hadi Ukraine, akithibitisha tena kwamba NATO haitakuwa sehemu ya mzozo huo.

Aidha amezihimiza nchi wanachama wa NATO kutoa misaada zaidi kwa Ukraine, akisema: "bado hatujachelewa sana kwa Ukraine kushinda. Tunahitaji kupeleka silaha zaidi na risasi kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga na silaha za masafa marefu".

Katika mahojiano hayo na gazeti la Ujerumani la Welt am Sonntag, Katibu Mkuu wa NATO amemzungumzia Rais Vladimir Putin wa Russia kwa kusema: "ikiwa Putin atapata anachokitaka Ukraine, hakutakuwa na usalama wa kudumu barani Ulaya, na ulimwengu kwa ujumla utazidi kuyumba".

Aidha amedai kwamba, sera ya kumridhisha rais huyo wa Russia haitakuwa na tija.../

 

 

Tags