Mzozo wa uchaguzi wa rais wa Marekani 2020 wafikishwa mahakamani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64443-mzozo_wa_uchaguzi_wa_rais_wa_marekani_2020_wafikishwa_mahakamani
Kama ilivyotazamiwa, uchaguzi wa rais wa Marekani umegeuka na kuwa malumbano makubwa ya kisiasa na sasa mzozo huo umetinga katika mahakama za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2020 07:12 UTC
  • Mzozo wa uchaguzi wa rais wa Marekani 2020 wafikishwa mahakamani

Kama ilivyotazamiwa, uchaguzi wa rais wa Marekani umegeuka na kuwa malumbano makubwa ya kisiasa na sasa mzozo huo umetinga katika mahakama za nchi hiyo.

Timu ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump aliyegombea urais wa tiketi ya chama cha Republican imewasilisha mashtaka kadhaa ikilalamikia zoezi la kuhesabu kura katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo. Timu hiyo inadai kuwa, maafisa wa uchaguzi katika baadhi ya majimbo likiwemo jimbo muhimu la Pennsylvania, hawawaruhusu wasimamizi wa uchaguzi wa chama cha Republican kukagua masanduku ya kura. Masaa 24 tu baada ya uchaguzi wa rais wa tarehe 3 Novemba, Rais Donald Trump wa Marekani alikariri katika ujumbe na matamshi yake kwamba kumefanyika udanganyifu mkubwa katika uchaguzi huo. Trump alisema waziwazi kwamba, atawasilisha mashtaka ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais katika Mahakama Kuu ya Federali. 

Malalamiko hayo ya kambi ya Donald Trump yametolewa wakati mpinzani wake katika uchaguzi huo, Joe Biden, alikuwa akikaribia kupata kura 270 za Electoral College zinazohitajika kuibuka mshindi katika kinyang'anyiro hicho. Biden hadi sasa amevunja rekodi ya kupata kura nyingi zaidi za wananchi katika uchaguzi wa rais wa Marekani na inatazamiwa kuwa atapata kura za kutosha za kumpa ufunguo wa Ikulu ya White House baada ya kukamilika zoezi la kuhesabiwa kura zote. 

Hata hivyo inaonekana kuwa mkazi wa sasa wa Wite House, (Donald Trump) hataki kabisa kukabidhi ufunguo kwa mrithi wake. Trump amekuwa akikariri kwamba atashinda uchaguzi huo la sivyo kutakuwa kumefanyika udanganyifu. Jitihada zake kubwa za kumteua jaji mhafidhina kupita kiasi wa Mahakama Kuu ya Federali zinatathminiwa katika mkondo huo. Trump anatarajia kwamba, atafanikiwa kuwashawishi majaji 6 kati ya 9 wa Mahakama Kuu ya federali ili wampasishe kubakia ndani ya ikulu ya White House. Suala hilo kwa kiasi fulani linawapa matumaini na utulivu wasimamizi wa timu ya uchaguzi ya Trump na waungaji mkono wa chama cha Republican.

Sahil Kapu ameandika katika ukurasa wa mtandao wa televisheni ya ABC kwamba: Wapiga kura wa chama cha repuiblican waliokuwa na wasiwasi kwamba yumkini Biden akaibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais, wamepata utulivu na matumaini ya kiasi fulani kwamba, Mahakama Kuu ya Federali yenye majaji wahafidhina itazima nia ya Wademocrat na kutwaa White House.

Miaka 20 iliyopita pia Mahakama ya Kuu ya Federali ilimsaidia mgombea wa chama cha Republican kwa kutoa hukumu ya kusimamishwa zoezi la kuhesabu kura za wananchi katika jimbo la Florida na hivyo kumtayarishia George W. Bush njia ya kuingia White House. Warepublican wanatarajia kwamba, mbinu hiyo hiyo itatumiwa tena mara hii dhidi ya wapiga kura waliowengi wa Marekani na kumbakisha Trump ndani ya White House.

Trump au Biden?

Hata hivyo mawakili wa timu ya uchaguzi ya Trump watalazimika kwanza kuwasilisha mashtaka yao kwenye mahakama za majimbo na baadaye katika Mahakama Kuu ya Federali. Hii ni pamoja na kuwa, haya yote yatategemea hoja na ushahidi utakaotolewa na timu ya Donald Trump kuhusiana na madai ya kufanyika udanganyifu katika zoezi zima la uchaguzi wa rais na katika kuhesabiwa kura hizo.

Hata hivyo inatupasa kuashiria hapa kwamba katika miezi ya karibuni Mahakama Kuu ya Federali ya Marekani imechukua maamuzi yanayopingana na matakwa ya chama cha Republican ikiwa ni pamoja na katika faili la kupokea kura za uchaguzi kupitia posta katika jimbo la Pennsylvania siku baada ya zoezi la uchaguzi licha ya kuwa na idadi kubwa ya majaji wahafidhina wanaokiunga mkono chama cha Republican. Kwa msingi huo yumkini mara hii pia mahakama hiyo isitoe hukumu kwa maslahi ya Trump katika mzozo wa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani.