Joe Biden atangazwa mshindi wa uchaguzi uliogubikwa na mizozo wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64493-joe_biden_atangazwa_mshindi_wa_uchaguzi_uliogubikwa_na_mizozo_wa_marekani
Hatimaye na baada ya siku nne za vuta nikuvute, vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden ndiye aliyechaguliwa na Wamarekani kuwa rais wa 46 wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2020 23:10 UTC
  • Joe Biden atangazwa mshindi wa uchaguzi uliogubikwa na mizozo wa Marekani

Hatimaye na baada ya siku nne za vuta nikuvute, vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden ndiye aliyechaguliwa na Wamarekani kuwa rais wa 46 wa nchi hiyo.

Ripoti zinasema kuwa Biden ameshinda kura 290 za wajumbe wa Electoral College baada ya kumpiku mpinzani wake, Donald Trump katika majimbo ya Pennsylvania na Nevada. Biden alihitajia kura 270 tu ya kati ya 538 za wajumbe wa Electoral College ili atangazwe mshindi. 

Timu ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump imesema bado ni mapema kumtangaza Joe Biden kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa tarehe 3 Novemba na kusisitiza kuwa, itawasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya jinsi zoezi la uchaguzi wa rais wa Marekani lilivyofanyika. Hata hivyo, kwa kutilia maanani ufa na tofauti kubwa iliyopo baina ya kura za wananchi na zile za wajumbe wa Electoral College za washindani hao wawili ni vigumu sana kuona matokeo yaliyotangazwa na vyombo vikuu vya habari vya Marekani yakibadilika kwa maslahi ya Donald Trump. Hivyo, tunaweza kusema kuwa, Biden ndiye atakayeshika hatamu za uongozi wa Marekani tarehe 20 Januari mwakani baada ya kipindi cha Donald Trump kumalizika rasmi. 

Joe Biden atashika hatamu za uongozi wa nchi inayosumbuliwa na matatizo mengi likiwemo janga la maambukizi ya coona, machafuko ya ubaguzi wa rangi na mpasuko mkubwa wa kisiasa na kijamii. 

Joe Biden

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, sababu kuu ya kushindwa Donad Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani ni kushindwa kukabiliana ipasavyo na maambukizi ya corona. Katika siku kadhaa zilizopita wakati wanasiasa wa Marekani walipokuwa wakitunishiana misuli kwa ajili ya kupata kura nyingi zaidi za wajumbe wa Electoral College, maambukizi ya virusi vya corona nchini humo yalipanda na kufikia watu laki moja na elfu 20 kwa siku moja, na idadi ya Wamarekani walioaga dunia kwa maradhi hiyo imepindukia watu laki mbili na 40 elfu. 

Kwa sasa mamilioni ya Wamarekani wamepoteza ajira zao kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na kazi nyingi zimefungwa. Nakisi ya bajeti ya Serikali ya Federali imefikia kiwango cha kutisha cha dola trilioni tatu, na deni la Serikali ya Federali limepindukia dola trilioni 27.

Sambamba na hayo, kwa miezi kadhaa sasa Marekani imekuwa katika lindi la ghasia na machafuko makubwa ya mgogoro wa ubaguzi wa rangi uliosababishwa na mauaji yaliyofanywa na polisi wazungu dhidi ya Wamarekani kadhaa weusi.

Vilevile migawanyiko ya kisiasa na kijamii katika nchi hiyo imefika kileleni kiasi cha baadhi ya wachambuzi wa mambo kutabiri uwezekano wa kutokea vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Hii ni pamoja na kuwa, kuendelea mzozo na mivutano ya Warepublican na Wademocrat juu ya matokeo ya uchaguzi wa rais uliomalizika siku chache zilizopita kunaifanya hali ya Marekani kuwa tete zaidi. Hali imekuwa mbaya sana kiasi kwamba watu kama John Bolton aliyewahi kuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Donald Trump wanasema: Usalama wa Marekani umedhoofika zaidi katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Trump kuliko ilivyokuwa kabla yake."

John Bolton (kulia) na Trump

Nje ya mipaka ya Marekani pia siasa za kigeni za nchi hiyo zimetawaliwa na hali shaghalabaghala. Kujiondoa Marekani katika makumi ya mikataba na makubaliano ya pande mbili, pande kadhaa na ya kimataifa katika kipindi cha uongozi wa Trump kumewakasirisha sana hata waitifaki wa serikali ya Washington. 

Vilevile siasa na sera zilizofeli za serikali ya Donald Trump mkabala wa nchi kama Russia, China, Iran, Venezuela na Korea Kaskazini zinamwachia rais ajaye rundo kubwa la matatizo yanayohitajia ufumbuzi. 

Ndani ya Marekani kwenyewe, Joe Biden anawajihiana na jamii iliyogawanyika, yenye hasira na vinyongo na iliyosawijika; huku nje ya mipaka ya nchi akikabiliana na nchi zilizokasirishwa na mienendo ya serikali ya Washington ya kukiuka ahadi na makubaliano yake na pande nyingine. 

Kutatua matatizo haya yote kutachukua nishati kuwa ya serikali ya baadaye ya Marekani. Hii ni pamoja na kuwa, bado haijulikani Biden atakuwa na uwezo kiasi gani wa kutimizia ahadi alizozitoa katika kampeni zake za uchaguzi.