Jan 10, 2021 08:18 UTC
  • Indonesia yathibitisha kuanguka baharini ndege iliyokuwa imebeba abiria 62

Wizara ya Uchukuzi ya Indonesia imethibitisha kuwa, ndege ya abiria ya nchi hiyo ambayo iliripotiwa kupoteza mawasiliano muda mfupi baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jakarta, imeanguka baharini ikiwa na abiria 62 wakiwemo watoto 10.

Akihutubia waandishi wa habari kwa njia ya intaneti jana jioni, Budi Karya Sumadi, Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo amesema ndege hiyo ya shirika la Sriwijaya Air yenye nambari ya usajili SJ-182 ilianguka baharini jana katika pwani ya Jakarta, muda mfupi baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Soekarno-Hatta huko Jakarta, mji mkuu wa nchi hiyo ikielekea mji wa Pontianak, mkoani Kalimantan, magharibi mwa nchi.

Juhudi za uokoaji zinaendelea kufanywa kujaribu kutafuta manusra wa ajali ya ndege hiyo ambayo iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Jakarta. Awali mashuhuda walisema wameiona ndege ikilipuka karibu na Kisiwa cha Pulau Laki nchini Indonesia.

Haya yanaripotiwa saa chache baada ya kuenea habari za ndege hiyo kupoteza mawasiliano muda mfupi baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jakarta. Ndege hiyo ya shirika la Boeing 737-500 la Marekani inaripotiwa kuwa imefanya kazi kwa miaka 26.

Baadhi ya wavuvi na wapiga mbizi wameoneshwa katika vyombo vya habari wakiwa wamebeba kile wanachokitaja kuwa mabaki ya ndege hiyo.

Moja ya ndege za shirika la Lion la Indonesia ilinguka zaidi ya 2 iliyopita

Ikumbukwe kuwa, Oktoba mwaka 2018, ndege nyingine ya abiria aina ya Boeing 737 ya shirika la ndege la Indonesia la Lion Air ilianguka kwenye bahari ya Java muda mfupi baada ya kuruka huku abiria wote 189 waliokuwemo ndani yake wakipoteza maisha.

Ajali hiyo ya mwaka 2018 inahesabiwa kuwa mbaya zaidi kutokea nchini Indonesia tangu ile ya Desemba 28 mwaka 2014 wakati ndege nyingine ya abiria ilipoanguka kwenye bahari ya Java. Abiria wote 162 waliokuwemo ndani yake walifariki dunia.

Tags