Canada yataka genge la Trump litambuliwe kuwa kundi la kigaidi
Bunge la Canada limeitaka serikali ya nchi hiyo liliweke rasmi genge la wanamgambo waliojizatiti kwa silaha na wafuasi sugu wa aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump katika orodha ya magenge ya kigaidi kama vile al-Qaeda na ISIS (Daesh).
Wabunge wa Canada hapo jana walipasisha kwa kishindo muswada unaoitaka serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu, Justin Trudeau kuliarifisha genge la 'Proud Boys' la Trump kama kundi haramu la kigaidi.
Genge hilo la kibaguzi linaloitakidi kuwa watu weupe ni bora kuliko watu wa jamii nyinginezo za Marekani limekuwa likimuunga mkono Trump kwa hali na mali katika kipindi chote cha utawala wake.
Mapema mwezi huu, Trump aliwachochea wafuasi wake hao kufanya fujo na mauaji katika Kongresi ya nchi hiyo. Mbali na kufanya mauaji na uharibifu, wafuasi hao sugu wa Trump pia walivunjia heshima maeneo mbalimbali nyeti ya Kongresi ikiwemo ofisi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi.
Wafuasi hao wa Trump walizusha ghasia hizo kwa lengo la kuzuia kikao cha Kongresi ya Marekani ambacho kilifanyika kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3 huko Marekani.
Wajumbe wa baraza la Seneti la Marekani wamepasisha kwa wingi wa kura muswada wa kushtakiwa Trump kwa kuchochea uvamizi na mauaji hayo. Kesi inayomkabili rais huyo wa zamani wa nchi hiyo itasikilizwa tarehe 8 mwezi ujao wa Februari katika baraza hilo.