Kuundwa serikali ya kijeshi nchini Myanmar baada ya mapinduzi ya kijeshi
Baada ya jeshi la Myanmar kufanya mapinduzi na kutwaa madaraka ya nchi, limetoa orodha ya majina ya watu 1 iliyowataja kuwa ndio watakaoongoza Baraza la Mawaziri la nchi hiyo.
Jeshi la Myanmar limetangaza katika taarifa yake kwamba, uchaguzi mpya wa Bunge utafanyika baada ya kipindi cha mpito cha mwaka mmoja ambapo katika muda huu kutakuwa na hali ya hatari nchini humo na kwamba, baada ya uchaguzi huo ndipo madaraka ya nchi yatakapobidhiwa kwa serikali mpya.
Jumatatu ya juzi ya tarehe Mosi Februari, jeshi la Myanmar lilitangaza kudhibiti madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi nchini Myanmar, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo ambayo ilizua hofu ya kutokea mapinduzi. Aidha Rais Win Myint wa Myanmar na viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa chama tawala pia walikamatwa hiyo juzi. Baada ya matukio hayo, jeshi la Myanmar limetangaza hali ya hatari kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambap kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.

Baada ya chama tawala cha NLD kudai kwamba, kimepata ushindi wa asilimia 83 wa viti vya Bunge, jeshi la Myanmar liliibuka na kukituhumu chama hicho kwamba, kimefanya udanganyifu na kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo na kuitaka Tume ya Uchaguzi kushughulikia madai hayo. Hata hivyo Tume ya Uchaguzi ya Myanmar ilitupilia mbali madai hayo ya jeshi na kueleza kwamba, uchaguzi huo ulikuwa salama.
Kwa mujibu wa Katiba ya Myanmar, asilimia 25 ya viti vya Bunge ni vya jeshi la nchi, kama ambavyo jeshi la nchi hiyo lina haki ya kikatiba ya kutangaza majina matatu kwa ajili ya nafasi za wizara.
Katika uchaguzi uliopita wa Bunge, chama chenye mfungamano na jeshi kiliambulia asilimia 6 tu ya viti vya Bunge, matokeo ambayo kwa mujibu wa maafisa wa jeshi, yatadhoofisha nafasi ya chombo hicho pamoja na katiba ya nchi. Ni kwa kutumia kisingizio hicho ndio maana jeshi la Myanmar lilitoa indhari kwamba, kama madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi hayatafanyiwa kazi, basi litachukua hatua.

Masaa machache baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar na kutiwa mbaroni viongozi wa chama tawala, haukupita muda mataifa kadhaa na asasi za kieneo na kimataifa zikaibuka na kutoa radiamali yao hasi kwa hatua hiyo ya jeshi, ambapo sanjari na kulaani uandamizaji huo wa demokrasia, zilitoa mwito wa kuachiliwa huru mara moja viongzoi waliotiwa mbaroni.
Kwa kuzingatia wigo mpana wa radiamali za nje dhidi ya mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar na mashinikizo tarajiwa kama kuwekewa vikwazo serikali iliyotokana na mapinduzi na hata uwezekano wa kusimamishwa uanachama wa nchi hiyo katika asasi za kieneo na kimataifa, filihahi kuna swali hili kwamba, je jeshi la Myanmar na serikali ya kijeshi vitakuwa na uwezo kiasi gani wa kukabiliana na mataukio yatakayofuatia baada ya mapinduzi hayo?
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, kikawaida serikali ambazo zinaingia madarakani kwa njia ya kijeshi katika nchi yoyote ile hukabiliwa na ghadhabu za kisiasa kimataifa na hata nchi ambazo zina uhusiano mzuri na nchi iliyoshuhudia mapinduzi nazo huchukua tahadhari katika ushirikiano wake wa kisiasa na kiuchumi na nchi hiyo.

Licha ya kuweko ukuruba mkongwe wa kisiasa na kiuchumi baina ya Myanmar na China hususan kuweko mshabaha wa kiutawala baina ya nchi hizo, lakini jeshi la Myanmar haliwezi kuwa na matumaini ya kupata himaya na uungaji mkono na ushirikiano wa Beijing kwa nchi hiyo katika kipindi cha baada ya mapinduzi ya kijeshi. Hii ni kutokana na kuwa, hivi sasa China haiko tayari kujiweka katika mazingira ya kutuhumiwa na madola ya Magharibi kwamba, inapuuza na kutoheshimu vigezo vya haki za binadamu na misingi ya demokrasia.
Ni kwa msingi huo, ndio maana weledi wa mambo wanatabiri kuwa, serikali ya sasa ya Myanamra ambayo ni zao la mapinduzi ya kijeshi, itakabiliwa na misukosuko na hali tete na yamkini mashinikizo ya ndani na ya nje yakaipigisha magoti na kulazimika kuhitimisha haraka hali ya hatari iliyotangaza na kuitisha uchaguzi haraka hata kabla ya muda iliyotangaza.