Malaki wameuawa katika operesheni za kijeshi za Marekani duniani
(last modified Fri, 26 Feb 2021 07:57:34 GMT )
Feb 26, 2021 07:57 UTC
  • Malaki wameuawa katika operesheni za kijeshi za Marekani duniani

Mamia ya maelfu ya watu wameuawa kutokana na uingiliaji wa kijeshi wa Marekani katika nchi mbalimbali duniani, tangu yalipojiri mashambulizi ya Septemba 11.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Watson ya Chuo Kikuu cha Brown imefichua kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu tu iliyopita, Marekani imefanya operesheni nyingi za kijeshi katika nchi 85 duniani, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Stephanie Savell, mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Brown amesema mbali na malaki ya watu kuuawa katika operesheni hizo za kijeshi za Marekani katika maeneo mbalimbali duniani, lakini wengine zaidi ya milioni 37 wameachwa bila makazi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, tangu Marekani ianze kufanya operesheni hizo baada ya tukio la Septemba 11 mwaka 2001, raia 335,745 wameuawa, na vilevile wanajeshi wa serikali 177,073, askari 12,468 wa vikosi waitifaki pamoja na wanajeshi 7,104 wa Marekani.

Mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani

Uingiliaji huo wa kijeshi wa Marekani usio na maana na ambao umegonga ukuta katika nchi tofauti duniani zikiwemo Afghanistan, Iraq, Yemen na Syria umewagharimu walipa kodi wa nchi hiyo dola trilioni 6.4.

Katika mashambulizi hayo ya Septemba 11 mwaka 2001 wanachama 19 wa kundi la kigaidi la al-Qaida waliteka nyara ndege nne za abiria na kuzitumia katika kushambulia maeneo kadhaa ya Marekani likiwemo jengo la Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon. Karibu watu 3,000 waliuawa katika hujuma hiyo. Baada ya mashambulizi hayo, Marekani ilizishambulia nchi za Iraq na Afghanistan. 

Tags