Mar 03, 2021 08:06 UTC
  • Russia: Marekani haina haki ya kuwafunza wengine akhlaqi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amekosa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo na kueleza kuwa, Marekani haina haki na haistahili kutoa darsa ya akhlaqi kwa nchi nyingine kutokana na hatua yake ya kujitoa kwa upande mmoja katika mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa yanayohusu kudhibiti na kupiga marufuku uenezaji wa silaha za maangamizi duniani.

Bi Maria Zakharova ameashiria vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Russia na kueleza kuwa, Marekani imechukua hatua hiyo kama kisingizio tu cha kuendeleza uingiliaji wake wa wazi katika masuala ya ndani ya Russia. Amesema Russia itatoa jibu kwa vikwazo hivyo dhidi yake. 

Zakharova amekosoa pia na kuyataja kuwa yasiyo na msingi madai ya Marekani kwamba, Alexei Navalny alipewa mada ya sumu inayotumika vitani na kwamba jambo hilo ndilo lililoipelekea Marekani kuiwekea Russia vikwazo vipya.  

Alexei Navalny, mpinzani wa serikali ya Russia anayeungwa mkono na Magharibi  

Ameongeza kuwa, mahesabu ya Marekani kwa ajili ya kuitwisha Russia matakwa yake kupitia vikwazo au kuishinikiza nchi hiyo yamegonga mwamba kitambo nyuma, na mara hii pia mahesabu hayo yataambulia patupu. 

Dimitry Peskov Msemaji wa Rais wa Russia pia jana Jumanne alitangaza kuwa, Kremlin ina imani kuwa, sera za vikwazo dhidi ya Russia hazitafikia malengo yake. Wizara ya Fedha ya Marekani jana iliziweka katika orodha yake nyeusi taasisi 14 kuhusiana na kesi ya Alexei Navalny mpinzani wa serikali ya Russia anayeungwa mkono na nchi za Magharibi. Itakumbukwa kuwa Mahakama nchini Russia hivi karibuni ilimhukumu kifungo cha miaka mitatu na nusu jela Alexei Navalny kwa kushindwa kutii sheria ya kuachiwa huru kwa masharti. 

Wakati huo huo maafisa saba wa ngazi ya juu wa Russia pia wamejumuishwa katika orodha hiyo ya vikwazo ya Marekani. Hadi sasa Marekani imeiwekea Russia karibu vifurushi 100 vya vikwazo. Marekani inachukau hatua hizi dhidi ya Russia tangu mwaka 2011.

Tags