Askari polisi aliyemuua Mmarekani mweusi, George Floyd apatikana na hatia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i69272-askari_polisi_aliyemuua_mmarekani_mweusi_george_floyd_apatikana_na_hatia
Derek Chauvin, afisa mzungu wa polisi wa Marekani ambaye alimuua kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd na kuzusha maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi dunia nzima hatimaye amepatikana na hatia katika mashitaka yote ya mauaji yaliyokuwa yakimuandama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2021 01:29 UTC
  • Askari polisi aliyemuua Mmarekani mweusi, George Floyd apatikana  na hatia

Derek Chauvin, afisa mzungu wa polisi wa Marekani ambaye alimuua kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd na kuzusha maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi dunia nzima hatimaye amepatikana na hatia katika mashitaka yote ya mauaji yaliyokuwa yakimuandama.

Baada ya kupita wiki tatu ya kufanyika vikao vya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka na mshtakiwa, jopo la majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo ya mauaji hayo jana Jumanne lilitangaza kuwa Chauvin amepatikana na hatia katika mashitaka matatu ya mauaji yaliyokuwa yakimuandama.

Hukumu dhidi ya afisa huyo mzungu wa Marekani inatazamiwa kusomwa katika kipindi cha wiki nane zijazo, na huenda atahukumiwa kifungo cha miongo kadhaa jela.

Hiyo jana kabla ya majaji kutoa tangazo la kumpata na hatia Chauvin mwenye umri wa miaka 45, maandamano makubwa yalikuwa yanaendelea nje ya mahakama na katika maeneo mengine ya mji wa Minneapolis.

Waandamanaji hao wanaojumuisha jamaa na marafiki wa Floyd pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wamepongeza uamuzi huo, wakisema kuwa huu ndio mwanzo wa safari ya kutokomeza ubaguzi wa rangi unaoisumbua jamii ya Wamarekani kwa miaka mingi. 

Chauvin akimkandamiza ardhini kwa goti Floyd

Afisa huyo mzungu alitiwa mbaroni tarehe 31 Mei mwaka jana kwa kosa la kumuua kikatili George Floyd katika mji wa Minneapolis huko Minnesota, magharibi mwa Marekani. 

Mkanda wa video ulioenea sana katika mitandao ya kijamii, ulimuonesha afisa huyo mzungu wa polisi akimdidimiza kwa goti hadi kumuua Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika, mchana kweupe mbele ya kadamnasi ya watu, huku muhanga wa ukatili huo akilalamika hawezi kupumua hadi alipokata roho.

Mauaji hayo yalizusha maandamano ndani na nje ya Marekani ya kupinga ubaguzi wa rangi chini ya kaulimbiu "Black Lives Matter."