Maiti 17 za wahajiri wa Kiafrika zapatikana katika kisiwa cha Uhispania
Miili 17 ya wahajiri wa Kiafrika imepatikana katika mji wa pwani wa El Hierro, ulioko katika moja ya visiwa vya Canary vya Uhispania.
Idara moja ya uokoaji katika eneo hilo imesema katika taarifa kuwa, maiti hizo zilipatikana jana Jumatatu zikiwa ndani ya boti, na kwamba manusura watatu (wanaume wawili na mwanamke mmoja) wamesafirishwa kwa helikopta ya jeshi la Uhispania na kupelekwa katika hopsitali moja iliyoko katika kisiwa cha Tenerife.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mmoja wa manusura yuko katika hali mbaya ya kiafya kutokana na kuishiwa na maji mwilini.
Msemaji wa Jeshi la Uhispania amesema wahajiri wote waliokuwemo kwenye boti hiyo ni raia wa nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara.
Amesema haijulikani ilikotokea boti hiyo, lakini ndege ya kijeshi ya nchi hiyo ya Ulaya iliigundua ikiwa umbali wa maili 265, kusini mashariki mwa mji wa pwani wa El Hierro.
Mapema mwezi huu, maiti nne zilipatikana ndani ya boti hafifu ya plastiki katika mji huo wa pwani wa El Hierro nchini Uhispania. Hata hivyo wahajiri 23 wa Kiafrika walinusuriwa na Gadi ya Pwani ya Uhispania katika tukio hilo.