May 11, 2021 02:50 UTC
  • Misikiti India yageuzwa kuwa vituo vya wagonjwa wa Covid-19

Aghalabu ya misikiti nchini India imegeuzwa na kuwa vituo vya kuwapokea wagonjwa wa Covid-19, huku mfumo wa afya wa nchi hiyo ukiendelea kulemewa kupita kiasi, vitanda kufurika mahospitalini, sambamba na kushuhudia uhaba mkubwa wa dawa na hewa ya oksijeni katika wimbi la pili la Corona nchini humo.

Kutokana na kurundikana wagonjwa mahospitalini na uhaba mkubwa wa vituo vya kuwapokea wagonjwa wa Corona nchini humo, misikiti na vituo vingi vya kidini vimeamua kuwa sehemu za kunusuru maisha ya wagonjwa hao japo kwa muda.

Mufti Arif Falahi, mkuu wa hauza ya kidini iliyoko katika mji wa Baroda katika jimbo la Gujarat la magharibi mwa nchi, amekigeuza kituo hicho cha kufunza elimu ya dini kuwa pahala pa kuokoa maisha ya wagonjwa wa Covid-19.

Ameiambia televisheni ya al-Jazeera kuwa, kwa siku wanalazimika kuwarejesha nyumbani watu kati ya 50 na 60, kwa kuwa kituo hicho kina uwezo wa kupokea watu 142 pekee na kuwapa huduma za hewa ya oksijeni.

Jana Jumatatu, watu 3,754 waliaga dunia kwa maradhi ya Covid-19 nchini India, huku idadi mpya wagonjwa wa Corona nchini humo ikipindukia 360,000. Kwa siku mbili mfululizo kabla ya jana, watu zaidi ya elfu nne waliaga dunia kwa ugonjwa huo kwa siku.

Janga la Corona linavyoisumbua India

Takwimu za Wizara ya Afya ya India zinaonyesha kuwa, watu 246,116 wameshapoteza maisha hadi sasa kwa COVID-19 nchini India huku wagonjwa waliothibitishwa kukumbwa na ugonjwa huo hadi hivi sasa katika nchi hiyo ya Asia wakipindukia milioni 22.

Baada ya Marekani ambayo imetangaza kuwa na wagonjwa zaidi ya milioni 33 wa Corona, India sasa imeshika nafasi ya pili duniani na kuipiku hata Brazil. 

Tags