May 16, 2021 12:07 UTC
  • Bunge la Cuba lautaka utawala wa Kizayuni uache kuwashambulia Wapalestina

Kamisheni ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Cuba imelaani jinai na mashambulio ya kikatili yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia na kuitaka Israel ikomeshe ukatili wake huo.

Shirika la habari la IRNA leo Jumapili limenukuu taarifa ya kamisheni hiyo ikisema kuwa, jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza kwa uungaji mkono kamili wa Marekani ni jambo linalopasa kulaaniwa na kila mwenye hisia za utu duniani.

Katika tamko lake hilo, kamisheni hiyo ya bunge la Cuba imewataka wawakilishi wa mabunge yote duniani pamoja na jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura na za haraka za kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai na mashambulizi yake dhidi ya watu wasio na hatia huko Palestina.

Wananchi wa Kenya katika maandamano ya kuiunga mkono Palestina

 

Kabla ya hapo pia, mamia ya maelfu ya wananchi wa Chile nao walikuwa wamendamana kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina. Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji na nchi mbalimbali duniani ukiwemo mji wa Mombasa, nchini Kenya.

Kwa upande wake, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Marekani, ambayo ni mmoja wa wanachama watano wenye haki ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikomeshe mlolongo wa kuikingia kifua Israel.

Ujumbe uliotumwa na Amnesty international katika mtandao wa Twitter umesema kuwa, shirika hilo linaitaka Marekani ilaani waziwazi jinai na uhalifu wa kivita na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa unaofanywa na Isarel ikiwa ni pamoja na kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na kulizingira eneo la Ukanda wa Ghaza. Vilevile iache kuikingia kifua na kuzuia hatua yoyote ya kuuadhibu utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendelea kukiuka sheria za kimataifa.

Tags