Russia inapanga mazoezi ya kijeshi na China, Belarus
https://parstoday.ir/sw/news/world-i73270-russia_inapanga_mazoezi_ya_kijeshi_na_china_belarus
Russia imepanga kufanya mazoezi mawili ya kijeshi mfululizo kwa kushirikiana na China na Belarus katika mipaka yake ya mashariki na magharibi ikijumuisha makumi ya maelfu ya wanajeshi wakati huu nchi hizo tatu zinahisi kuwa zinakabiliwa na tishio kutoka Marekani na muungano wa kijeshi wa NATO.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2021 03:08 UTC
  • Russia inapanga mazoezi ya kijeshi na  China, Belarus

Russia imepanga kufanya mazoezi mawili ya kijeshi mfululizo kwa kushirikiana na China na Belarus katika mipaka yake ya mashariki na magharibi ikijumuisha makumi ya maelfu ya wanajeshi wakati huu nchi hizo tatu zinahisi kuwa zinakabiliwa na tishio kutoka Marekani na muungano wa kijeshi wa NATO.

Kwa mujibu wa taarifa, mazoezi ya kwanza - yaliyopewa jina la Zapad-Interaction, 2021, yanatarajiwa kuanza kuanza Jumatatu katika Kituo cha Mafunzo ya Pamoja cha Qingtongxia kaskazini magharibi mwa China katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Ningxia.

Mazoezi hayo ya pamoja yalitangazwa wiki iliyopita na maafisa wa jeshi la Russia na China, na yatashirikisha askari wasiopungua 10,000 na silaha na vifaa anuwai kutoka pande zote mbili.

Kulingana na ripoti hiyo, mazoezi haya ni ya nne ya kimkakati ya pamoja ya China na Russia na ya kwanza kufanyika nchini China.

Katika taarifa kuhusu mazoezi hayo, Jeshi la China limesema wanajeshi wa China na Urusi watafanya mazoezi pia kuhusu mbinu za kukabiliana na magaidi.

Beijing na Moscow zimeimarisha uhusiano wao wa kijeshi na kiufundi katika miaka ya hivi karibuni, na ushirikiano huo ulitiliwa mkazo mwezi uliopita wakati washirika hao wawili waliposherehekea kumbukumbu ya miaka 20 ya Mkataba wa Russia-China wa Ujirani mwema na Ushirikiano wa Kirafiki.

Mazoezi ya kijeshi

Kuanzia Septemba 10, mazeozi mengine yaliyopewa jina la "Zapad" yatafanyika Belarus. Inatazamiwa kuwa wanajeshi 13,000 - kutoka Belarus - na wengine 2,500 kutoka Russia watashiriki. Belarus ni mshirika mkuu wa Moscow kwenye mpaka wa magharibi wa Russia. Serikali ya Belarus inaituhumu Marekani na wanachama wa karibu wa NATO Latvia na Poland kuwa wanapanga njama za kuchochea machafuko nchini humo.