Wanasayansi watahadharisha kuhusu uhaba wa chakula utakaoikumba dunia miongo miwili ijayo
Wanasayansi wametahadharisha kuwa uzalishaji wa chakula duniani kote utapungua kutokana na kuongezeka joto la sayari ya dunia kwa nyuzijoto 1.5 selsiasi. Hii ni kufuatia ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu baa la mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, kufuatia ripoti ya sita ya tathmini ya Umoja wa Mataifa, wanasayansi wametahadharisha kuwa, kuongezeka joto la sayari ya dunia kutakuwa na taathira kubwa katika kudhamini mahitaji ya chakula katika kipindi cha miongo miwili ijayo.
Kwa upande mwingine, wanasiasa mbalimbali duniani nao pia wametoa maoni yao kuhusiana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametoa mkanda wa video akiashiria mpango wa maeneo manne ambayo amesema yatafanyiwa kazi hadi kitakapofanyika kikao cha msimu wa mapukutiko kuhusu tabianchi.
Mpango huo wa Johnson unajumuisha kupiga marufuku ifikapo mwaka 2040 uzalishaji umeme kwa kutumia nishati ya makaa ya mawe pamoja na fueli ya fosili, kuzishawishi nchi zenye uwezo kuzisaidia nchi masikini sambamba na mabadiliko ya tabianchi na kukomesha uharibifu wa misitu.
Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye anakabiliwa na mashinikizo ya kumtaka apitishe sheria kuhusu mabadiliko ya tabianchi amesema "haiwezekani kukaa na kungojea tu hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi irekebishike yenyewe kwa yenyewe."
Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison yeye ameituhumu China kwa kusema, "haiwezekani kupuuza suala kwamba nchi zinazoendelea ndizo zinazohusika na usambaaji wa theluthi mbili ya gesi ya sumu ya kijani".
Hata hivyo serikali ya Beijing imejibu tuhuma hizo kwa kusema, nchi hiyo inatilia mkazo kutoa kipaumbele kwa ustawi endelevu, wa mazingira kijani na kupunguza kiwango cha dioksini ya kaboni.
Wasiwasi juu ya suala la hifadhi ya mazingira sasa limekuwa suala lenye kupewa uzito mkubwa kiusalama katika mahusiano ya kimataifa na kuwashughulisha mno viongozi wa nchi mbalimbali.../