Facebook yatakiwa kufuta matangazo ya AIPAC yanayoeneza chuki dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i73558-facebook_yatakiwa_kufuta_matangazo_ya_aipac_yanayoeneza_chuki_dhidi_ya_waislamu
Mtandao wa kijamii wa Facebook uko chini ya shinikizo yanayoutaka kuondoa matangazo yanayohujumu Uislamu na Waislamu dhidi ya mwakilishi Muislamu wa Kongesi ya Marekani Ilhan Omar, ambayo vikundi vya wanasheria vinasema yanahatarisha maisha ya mbunge huyo wa Minnesota.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 16, 2021 02:38 UTC
  • Facebook yatakiwa kufuta matangazo ya AIPAC yanayoeneza chuki dhidi ya Waislamu

Mtandao wa kijamii wa Facebook uko chini ya shinikizo yanayoutaka kuondoa matangazo yanayohujumu Uislamu na Waislamu dhidi ya mwakilishi Muislamu wa Kongesi ya Marekani Ilhan Omar, ambayo vikundi vya wanasheria vinasema yanahatarisha maisha ya mbunge huyo wa Minnesota.

Ni baada ya Kamati ya Masuala ya Umma ya Marekani na Israeli (AIPAC), ambacho ni kikundi kinachounga mkono Israeli huko Marekani, kutumia kwa muda mrefu mbinu za unyanyasaji na vitisho ili kuwanyamazisha wakosoaji wa utawala wa wa Kizayuni wa Israeli ndani ya Kongresi na kuwazuia kutetea haki za binadamu za Wapalestina.

Katika siku za karibuni AIPAC imekuwa ikiendesha matangazo ya hujuma na mashambulizi kwenye mtandao wa Facebook dhidi ya Mwakilishi Ilhan Omar, mkosoaji mkuu wa utawala wa Israeli, ikimtuhumu kuwa "hatofautishi kati ya Marekani na Taliban" na kati ya "demokrasia na magaidi."

Siku ya Jumatano iliyopita, Jeremy Slevin, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bunge la Kongresi ya Marekani, alilaani matangazo hayo na akasema lugha inayotumiwa na AIPAC "inafanana" na ujumbe wa chuki ambao Omar amekuwa akiupokea mara kwa mara. Ameongeza kuwa "AIPAC inaweka hatarini maisha ya mbunge Ilhan Omar kwa matangazo ya hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislam ."

Wakati huo huo jumuiya ya CodePink inayopinga sera za vita za Marekani dhidi ya nchi mbalimbali imeitaka Facebook kufuta matangazo yanayochochea chuki dhidi ya Uislamu.

Taarifa na Ariel Gold, mkurugenzi mwenza wa CodePink imesema: "Uchochezi na hujuma inayolenga Waislamu inayofanywa na AIPAC dhidi ya mwanamke wa Kiislamu mwenye asili ya Afrika katika Kongresi ili kuendeleza ajenda yake inayounga mkono Israeli, ni aibu na ni hatari."

Gold ameongeza kuwa "licha ya mashambulio dhidi yake tangu alipoingia bungeni, Ilhan Omar ameendelea kwa ujasiri kupaza sauti yake ya kutetea haki za Wapalestina wanaoishi chini ya mfumo wa kikatili wa Israeli na ubaguzi wa rangi".

Ilhan Omar

Taarifa ya CodePink imesema: "Ikiwa kitu chochote kitamtokea mbunge Omar, AIPAC na Facebook zitakuwa washirika katika uhalifu huo kwa kuruhusu matangazo ya kichochezi."

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu na America (CAIR), ambalo ni shirika la kutetea haki za raia lenye makao yake Washington, pia limetoa taarifa likilaani harakati za kundi la mashinikizo la Wayahudi wa Marekani, AIPAC kwa "kampeni yake ya matangazo yanayohujumu Uislamu dhidi ya Ilhan Omar. 

CAIR pia imetaka Facebook kufuta matangazo hayo ya AIPAC.

Ilhan Omar amekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili na mienendo ya kibaguzi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.