Washington Examiner: Joe Biden anakimbia Afghanistan
Mtandao wa habari wa Washington Examiner umejadili kadhia ya Afghanistan kwa makala yenye kichwa cha habari: "Joe Biden anakimbia Afghanistan" na kusema, Marekani imejidanganya na kuona ndoto huko Afghanistan.
Ripoti ya Washington Examiner inasema Joe Biden alitangaza tarehe 31 Agosti kuwa ndio utakaokuwa mwisho wa kuwepo majeshi ya nchi hiyo huko Afghanistan kabla ya kumbukumbu ya mashambulizi ya Septemba 11 na hakuamini kwamba Taliban wataidhibiti tena nchi hiyo wala hakudhani kuwa tarehe 15 mwezi huu wa Agosti Kabul itakuwa Saigon nyingine kwa Marekani.
Jumapili ya tarehe 15 Agosti, wapiganaji wa kundi la Taliban waliingia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, hatua iliyofuatiwa na rais wa nchi hiyo Muhammad Ashraf Ghani kuitoroka nchi.
Baada ya kuingia mjini humo, kundi la Taliban lilishika hatamu za udhibiti wa idara za serikali na vituo vya polisi vilivyoachwa na vikosi vitiifu kwa serikali ya Ashraf Ghani.
Kufuatia wapiganaji wa Taliban kuingia mjini Kabul, maelfu kwa maelfu ya watu walikimbilia uwanja wa ndege wa kimataifa ulioko katika mji huo kwa madhumuni ya kuihama nchi.
Taasisi ya Watson Institute for International and Public Affairs katika Chuo Kikuu cha Brown imetangaza katika ripoti yake mpya kwamba, Marekani imetumia dola trilioni 2.26 katika vita vyake vya miaka 20 huko Afghanistan ambavyo vilianza msimu wa mapukutiko wa mwaka 2001.
Ripoti hiyo inayohitimisha vibaya sana faili la vita na uvamizi wa miongo miwili wa Marekani huko Afghanistan ambako wanajeshi wa nchi hiyo wameondoka kwa njia inayoshabihiana na ile ya kukimbia kwa fedheha wanajeshi wa Marekani huko Saigon nchini Vietnam, inafungua ukurasa mwingine wa kashfa na fedheha ya Washington huko Afghanistan.