Ombi la kiongozi wa Taliban kwa wananchi wa Afghanistan
Hibatullah Akhundzada kiongozi mkuu wa kundi la wanamgambo wa Taliban amewataka wananchi wa Afghanistan kuiunga mkono serikali ya mpito ya kundi hilo. Amesema, Afghanistan ni nyumba ya taifa lote la Afghanistan na kwamba nyumba hiyo ni muhimu katika kuijenga nchi.
Kuna nukta kadhaa kuu na za kuzingatia kuhusu ombi hilo la Hibatullah Akhundzada kwa wananchi wa Afghanistan. Ya kwanza ni kuwa, mwaka uliopita kulienezwa taarifa za kuaga dunia kiongozi huyo mkuu wa Taliban kwa ugonjwa wa COVID-19. Pili ni kwamba, lugha iliyotumiwa katika taarifa hiyo inaonyesha kuwa, imetayarishwa na kuandikwa na upande wenye uwezo na weledi mkubwa zaidi ya viongozi wa Taliban, na baadhi ya duru zinasema imetayarishwa na Shirika la Ujasusi la Jeshi la Pakistan (ISI).
Pamoja na hayo malalamiko na maandamano ya wananchi wa Afghanistan yanaonyesha kuwa, hatua za kundi la Taliban katika karibu siku 20 zilizopita tangu kundi hilo lilipoudhibiti mji wa Kabul zimeshindwa kuwashawishi raia wa nchi hiyo na zimesababisha wasiwasi katika duru za kieneo na kimataifa. Hii ina maana kuwa, kundi la Taliban linapasa kuweka wazi iwapo linazungumza na wananchi wa Afghanistan kama kundi la wanamgambo wanaobeba silaha au kama kundi linalowajibika ambalo linatarajia kusimamia na kuongoza mustakbali wa Afghanistan. Matamshi ya Muhammad Hassan Akhund Rais wa serikali ya mpito ya Taliban kwamba umwagaji damu umemalizika pia yanayonyesha kuwa, Taliban wanaendelea kuzungumza na wananchi wa Afghanistan kama kundi la wanamgambo wenye silaha.
Nargis Etemad mchambuzi wa masuala ya kisiasa huko Afghanistan anasema: "Uongozi wa Taliban unapasa kukabiliana kiuwajibikaji na mtihani huu mkubwa. Taliban inapasa kukidhi matakwa ya wananchi wa Afghanistan na kujua kwamba, kuna tofauti baina ya nara tupu na matendo. Kinyume chake, kundi la Taliban linapasa kusubiri upinzani wa wananchi wa Afghanistan.
Baada ya kuudhibiti mji Kabul, kundi la Taliban liliwaahidi wananchi kwamba litaunda serikali jumuishi na kulinda haki zao. Hata hivyo matamshi ya uongozi wa kundi hilo kwamba watatekeleza sharia kwanza kabla ya kuzingatia haki za wananchi, kaumu na madhehebu mbalimbali nchini Afghanistan, yamezidisha wasiwasi kuhusu utendani wa Taliban. Kundi hilo linadai kuwa, hivi sasa limebadilika na lina lengo la kuunda serikali yenye uwezo wa kuijenga Afghanistan yenye maendeleo na hali bora ya maisha kwa wananchi. Pamoja na hayo tunapasa kuzingatia nukta muhimu kwamba, wananchi wa Afghanistan watakuwa tayari kushirikiana na serikali iliyotangazwa na kundi la Taliban pale kundi hilo litakapochukua hatua za kulifanya likubalike na kuaminiwa miongoni mwa jamii yenye kaumu, madhehebu na makundi tofauti ya Afghanistan. Hata hivyo jambo hilo haliwezi kutimia bila ya kuheshimu na kuzingatia haki na matakwa ya wananachi wa Afghanistan hususan wanawake ambao wanaunda sehemu kubwa ya jamii ya nchi hiyo.
Maandamano yaliyofanywa ndani ya Afghanistan baada ya kundi la Taliban kutangaza serikali yake ya muda na wasiwasi uliojitokeza kieneo na kimataifa yote hayo yanaonyesha kuwa, kundi hilo limezuia kikamilifu ushirikiano wa aina yoyote na wananchi. Kwa msingi huo, serikali ya Pakistan ambayo inafanya kila iwezalo ili kuhakikisha kunakuwepo ushirikiano wa kieneo na kimataifa na Taliban, kabla ya chochote kile, inapasa kulishawishi kundi hilo litekeleza ahadi zake hususan kuhusu suala la kuasisi serikali jumuishi ya makundi na vyama vyote vya Afghanistan.
Asef Ashna mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anasema: Taliban imebadilika kisiasa na kuwa tofauti na Taliban ya miaka ya nyuma; hata hivyo kwa upande wa itikadi Taliban bado ni ile ile ya zamani, na hilo linakinza waziwazi na ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afghanistan katika miongo miwili iliyopita.