China; changamoto kubwa zaidi ya Marekani ya 'jeostratijia'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76302-china_changamoto_kubwa_zaidi_ya_marekani_ya_'jeostratijia'
Mkuu wa majeshi ya Marekani, Mark Milley amesema kuwa, ametiwa wasiwasi na jaribio la hivi karibuni la kombora la kisasa la China linalozidi kasi ya sauti.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 29, 2021 05:14 UTC
  • China; changamoto kubwa zaidi ya Marekani ya 'jeostratijia'

Mkuu wa majeshi ya Marekani, Mark Milley amesema kuwa, ametiwa wasiwasi na jaribio la hivi karibuni la kombora la kisasa la China linalozidi kasi ya sauti.

Jenerali Milley amekiri kuwa uwezo wa kijeshi wa China ni mkubwa mno kuliko inavyodhaniwa na kusisitiza kuwa, China ndiyo changamoto kubwa zaidi ya jeostratijia kwa Marekani na kwamba hana shaka hata kidogo kuhusu suala hilo. Afisa huyo wa ngazi za juu kabisa wa jeshi la Marekani vile vile amesema: "Maendeleo ya China ni ya kipekee na sijapata kuona. Wachina wameunda jeshi kubwa na lenye nguvu sana."

Mtazamo huo wa mkuu wa majeshi ya Marekani kuhusu China na kukiri kwake kwamba nchi hiyo ndio changamoto kubwa zaidi ya jeostratijia kwa Marekani katika karne ya 21, kwa hakika ni ushahidi wa mtazamo mkuu wa Washington kuhusu ushawishi na nguvu za China katika eneo la Indo-Pasifiki na pia katika upeo wa kimataifa.

Jenerali Mark Milley

Serikali ya Joe Biden imeamua kufuata siasa za mashambulio kukabiliana na wapinzani wake kimataifa yaani China na Russia. Hati ya "Muongozo wa Muda wa Stratijia ya Usalama wa Taifa" ya serikali ya Joe Biden iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu wa 2021, imetamka wazi kuwa tishio kubwa zaidi la Marekani ni madola mawili ya kimataifa ya Mashariki na Eurasia yaani China na Russia. Hata hivyo matamshi chungu nzima ya wakuu wa ngazi za juu wa Marekani yanaonesha kuwa, kwa mtazamo wa serikali ya Biden, tishio kubwa zaidi kwa Marekani ni Jamhuri ya Watu wa China. Ukweli ni kwamba kwa kuingia madarakani Joe Biden huko White House, si tu ugomvi baina ya China na Marekani haujapungua, lakini pia vita baridi baina ya nchi hizo mbili vimepamba moto na kuleta wasiwasi kwa usalama wa dunia nzima.

Hati ya kiusalama ya serikali ya Biden, yaani "Muongozo wa Muda wa Stratijia ya Usalama wa Taifa" imegusia kuongezeka ushawishi na nguvu za China kimataifa na kutamka wazi kuwa, Beijing ndiye mpinzani pekee ambaye anaweza kutumia kwa pamoja nguvu za kiuchumi, kidiplomasia, kijeshi na kiteknolojia kuleta changamoto ya kudumu katika mfumo uliotulia wa kimataifa.

Eneo la Bahari ya China Kusini

Maneno makali ya viongozi wa Marekani yamejikita kwenye kulaumu hatua za China katika nyuga tofauti za kiuchumi, kibiashara, kijeshi, kiusalama na haki za binadamu na hivi sasa wanaonesha wazi kuwa ajenda kuu ya Washington ni kuidhibiti China kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo za kushirikiana na waitifaki wa White House. Marekani inadai kuwa, hatua zilizochukuliwa na China katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni hasa katika bahari ya kusini mwa China zimehatarisha usalama wa safari za vyombo vya majini vya nchi za eneo hilo. Aidha hivi sasa China inaendelea kwa kasi na mradi wake wa kujenga visiwa vipya baharini kwa ajili ya kupanua eneo lake la utawala na kujiimarisha kiuchumi na kiistratijia kusini mwa nchi hiyo. Sasa ili kukabiliana na China, Marekani imeamua kuongeza uwepo wake wa kijeshi na wa waitifaki wake katika bahari ya kusini mwa China. Pamoja na hayo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, Marekani haiwezi kupambana na China katika vita vya pande zote licha ya Washington kutumia fedha nyingi sana kujiimarisha kijeshi. 

Admiral Philip S. Davidson, mkuu wa zamani wa kikosi cha majini cha Marekani katika eneo la Indo-Pasifiki anasema: Katika kipindi cha miaka sita ijayo, jeshi la China litakuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko Marekani na jambo hilo litalazimisha kuangaliwa upya misimamo na hali halisi ya mambo katika eneo la mashariki mwa Asia.

Tab'an wakati wa urais wa Joe Biden, Marekani imeonesha wazi kuwa haitobadilisha siasa zake na itaendelea kushirikiana na waitifaki wa Washington kupambana na vitisho inavyodai vinasababishwa na China katika eneo la Indo-Pasifiki. Mkataba wa pande nne ujulikanao kwa jina la  QUAD baina ya Marekani, Australia, Japan na India, na muungano wa nchi tatu za Marekani, Uingereza na Australia uitwao AUKUS ni katika siasa hizo za Marekani za kukabiliana na China kwa gharama yoyote ile.

Admiral Philip S. Davidson