Changamoto zinazomsubiri Olaf Scholz, Kansela mpya wa Ujerumani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i77840-changamoto_zinazomsubiri_olaf_scholz_kansela_mpya_wa_ujerumani
Jumatano tarehe 8 Disemba 2021, Bunge la Ujerumani ambalo linajulikana kwa jina la Bundestag lilimchagua Olaf Scholz, 63, kuwa Kansela mpya wa nchi hiyo ya Ulaya. Scholz alipata kura 395 za ndio kati ya kura zote 736 wa wabunge wa nchi hiyo, na hivyo kufanikiwa kurithi kiti cha Angela Merkel ambaye ameitawala Ujerumani kwa muda wa miaka 16.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2021 01:08 UTC
  • Changamoto zinazomsubiri Olaf Scholz, Kansela mpya wa Ujerumani

Jumatano tarehe 8 Disemba 2021, Bunge la Ujerumani ambalo linajulikana kwa jina la Bundestag lilimchagua Olaf Scholz, 63, kuwa Kansela mpya wa nchi hiyo ya Ulaya. Scholz alipata kura 395 za ndio kati ya kura zote 736 wa wabunge wa nchi hiyo, na hivyo kufanikiwa kurithi kiti cha Angela Merkel ambaye ameitawala Ujerumani kwa muda wa miaka 16.

Lars Haider, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Ujerumani amesema, Olaf Scholz amechaguliwa kuwa kansela mpya wa Ujerumani kutokana na shakhsia yake kufanana mno na ya Angela Merkel. Suala hilo limekuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa Scholz kuwa kansela mpya wa nchi hiyo.

Muungano wa vyama vitatu ndio unaunda serikali ya Ujerumani hivi sasa navyo ni vya Social Democrat, Liberal Democrat na Chama cha Kijani. Baada ya kufanyika mazungumzo mazito na ya kina, vyama hivyo vitatu vimeamua Scholz achaguliwe kuwa kansela mpya wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa katika uchaguzi wa Bunge wa mwezi Septemba mwaka huu wa 2021, chama cha Social Democrat kilishika nafasi ya kwanza kwa kupata asilimia 25 ya kura na hii ni mara ya kwanza katika historia ya Ujerumani, kuwa na serikali iliyoundwa kwa ushirika wa vyama vitatu yaani hicho cha Social Democrat pamoja na kile cha Kijani na cha Liberal Democrat, tab'an vyama hivyo vitatu vina hitilafu nyingi kubwa baina yao. Muungano unaounda serikali ya hivi sasa ya Ujerumani umepewa lakabu ya taa ya kuongozea njia kutokana na rangi za vyama vinavyounda serikali hiyo yaani nyeusi, njano na kijani. 

Bunge la Ujerumani, Bundestag

 

Baada ya Scholz kutangazwa kuwa kansela mpya wa Ujerumani, sasa serikali hiyo mpya imeelekeza jicho lake kwenye changamoto na masuala mbalimbali ya ndani ya nchi hiyo. Changamoto muhimu zaidi kwa hivi sasa ni kupambana na janga la UVIKO-19 ambalo hivi sasa idadi ya maambukizi na wahanga wa ugonjwa huo wa corona imeongezeka vibaya huko Ujerumani. Jengine ni kwamba kila chama kati ya vyama vitatu vinavyounda serikali mpya ya Ujerumani kina daghadagha na wasiwasi wake na kila kimoja kina mtazamo wake kuhusu masuala ya ndani ya Ujerumani hasa katika suala la kulinda mazingira ambalo ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa na chama cha Kijani.

Katika upande wa ustawi wa jamii pia, kutokana na madhara makubwa yaliyosababishwa na janga la corona katika uchumi wa Ujerumani, na maisha ya wananchi wa nchi hiyo, hakutakuwa na uwezekano wa kuongeza sana mishahara ya wafanyakazi. 

Amma kuhusu wakimbizi, Ujerumani inahitaji kuwa na mpango maalumu mkuu na amilifu wa kuweza kushughulikia suala la wakimbizi na jambo hilo ni muhimu kwa vyama vitatu vinavyounda serikali mpya ya Ujerumani. Makubaliano yaliyofikiwa baina ya vyama hivyo vitatu, vimeifanya Ujerumani kwa mara ya kwanza kuhesabiwa kuwa na jamii yenye watu wa kila aina wanaoundwa na "uhajiri na wahajiri."  Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kuanzia sasa, wageni watakaoishi kwa muda wa miaka mitano nchini Ujerumani watakuwa na haki ya kupewa uraia wa nchi hiyo.

Olaf Scholz, kansela mpya wa Ujerumani aliyechukua nafasi ya Angela Merkel

 

Amma katika upande wa Ulaya na kwa kuzingatia kuwa chama cha Social Democrat  kinalipa umuhimu mkubwa suala la ushirikiano baina ya nchi za bara hilo, inatarajiwa kuwa serikali mpya ya Ujerumani inaongeza bidii za kuimarisha ushirikiano huo na vile vile kukabiliana na hatua zinazochukuliwa na nchi kama Hungary na Poland.

Amma kuhusu uhusiano wa Ujerumani na maeneo ya nje ya Atlantiki tunaweza kutabiri kwamba, kansela mpya wa Ujerumani atachukua misimamo mikali zaidi kuliko kansela aliyemtangulia yaani Angela Merkel. Kansela mpya wa Ujerumani ni katika wapinzani wakuu wa uamuzi uliochukuliwa na rais wa Marekani, Joe Biden wa kuondoa wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan hatua ambayo ilipelekea wanajeshi wa NATO nao waondoke nchini humo. Inatarajiwa pia kuwa, wakati wa utawala wa Olaf Scholz, suala la kuwekwa silaha za nyuklia za Marekani huko Ujerumani litajadiliwa upya. Kuna uwezekano pia kwamba serikali mpya ya Ujerumani itaitaka Marekani iondoe mabomu yake ya nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo. Ingawa jambo hilo linaungwa mkono na wananchi wa Ujerumani, lakini bila ya shaka yoyote litazidisha ufa baina ya wanachama wa NATO.