Makumi wauawa katika maandamano ya fujo Kazakhstan
(last modified Thu, 06 Jan 2022 13:32:24 GMT )
Jan 06, 2022 13:32 UTC
  • Makumi wauawa katika maandamano ya fujo Kazakhstan

Makumi ya watu wameuawa katika makabiliano baina ya waandamanaji na maafisa usalama nchini Kazakhstan, huku maandamano ya ghasia yakichachamaa katika nchi hiyo ya Asia ya Kati.

Msemaji wa Polisi ya nchi hiyo, Saltanat Azirbek amesema makumi ya wafanya fujo wameuawa na maafisa usalama katika maandamano ya jana na leo katika mji mkuu wa kiuchumi wa Almaty, walipojaribu kushambulia majengo yenye ofisi za serikali.

Azirbek amewataka wananchi kusalia majumbani mwao, huku operesheni ya kuzima maandamano hayo ya ghasia na umwagaji damu ikishika kasi.

Mkuu wa Polisi katika jiji la Almaty, Kanat Taimerdenov, amesema wanaofanya fujo na kuharibu mali za umma, mbali na kushambulia wananchi wenzao kwenye maandamano hayo ni watu wenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Maafisa usalama wakikabiliana na waandamanaji Kazakhstan

Kwa siku kadhaa sasa, wananchi wa Kazakhstan wamekuwa wakifanya maandamano ya kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta. Maandamano hayo yaliibuliwa na madereva Jumapili iliyopita katika mji wa Zhanaozen katika eneo la Mangystau.

Ifahamike kuwa, nchi hiyo ya katikati mwa bara Asia ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa mafuta duniani.