Serikali: Watu waliouawa katika ghasia za Kazakhstan ni 225
(last modified Sun, 16 Jan 2022 07:56:00 GMT )
Jan 16, 2022 07:56 UTC
  • Serikali: Watu waliouawa katika ghasia za Kazakhstan ni 225

Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Kazakshtan imesema watu 225 wakiwemo maafisa usalama 19 wameuawa katika machafuko ya hivi karibuni katika nchi hiyo ya Asia ya Kati.

Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na ofisi hiyo ya serikali ya Kazakhstan imeeleza kuwa, mbali na watu 225 kuuawa, wengine wapatao 4,353 wakiwemo maafisa usalama 3,393 walijeruhiwa katika ghasia hizo zilizoanza Januari 2.

Wakazaki hao waliuawa katika makabiliano ya siku kadhaa baina ya waandamanaji na maafisa usalama. Wananchi wa Kazakhstan walianzisha maandamano ya kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta,na muda mfupi baadaye yaligeuka na kuwa maandamano ya fujo.

Ghasia hizo zimelisababishia taifa hilo hasara ya takriban dola milioni 200, kushambuliwa na kuibiwa benki na maeneo ya biashara, mbali na kuchomwa moto magari zaidi ya 400.

Hata hivyo kwa sasa hali ya utulivu, nidhamu na utawala wa kikatiba imerejeshwa katika maeneo karibu yote ya nchi hiyo, lakini operesheni za kupambana na kile ambacho serikali imekitaja kuwa 'ugaidi' zingali zinaendelea.

Rais Kassym-Jomart Tokayev wa nchi hiyo ambaye alikuwa ametoa amri ya kuuawa kwa kupigwa risasi wafanya fujo, ametangaza kuondoa hali ya hatari katika maeneo ya Akmola na Kostanay, na kupelekea idadi ya majimbo yaliyoondolewa kwenye hali ya hatari kufikia 10.