Kulalamikiwa vitendo vya kibaguzi vya Uingereza dhidi ya Waislamu
Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya nchini Uingereza imeulalamikia vikali uamuzi wa kibaguzi wa saerikali ya nchi hiyo wa kuunda timu ya kuchunguza namna ya utekelezaji wa sheria na kanuni za Kiislamu nchini humo.
Tamko la kamisheni hiyo lililotolewa Alkhamisi usiku limesema, kitendo cha serikali ya Uingereza cha kuunda timu maalumu ya kuchunguza namna ya utekelezaji wa hukumu za Kiislamu nchini humo ni mfano mwingine wa siasa za chuki za serikali hiyo na namna inavyowabagua Waislamu. Itakumbukwa kuwa siku ya Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Theresa May, aliliandikia barua bunge la nchi hiyo na kulitaaribu kuundwa kamati huru ya kuchunguza namna ya utekelezaji wa sheria za Kiislamu na madhara yake kwa Uingereza. Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza aidha imesema katika taarifa yake kuwa, madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza ya kuhalalalisha kitendo chake hicho hayakubaliki. Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Uingereza alidai kuwa mabaraza ya sheria za Kiislamu hayafai na yanafanya ubaguzi nchini Uingereza. Hata hivyo waziri huyo ameshindwa kutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake hayo kama ambavyo amekwepa pia kujibu swali la kwa nini tume hiyo imeundwa kwa ajili ya kuzichunguza taasisi za Waislamu tu? Tamko la Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza limeongeza kuwa, jamii ya Mayahudi waishio Uingereza ina mahakama zake maalumu za kutatua hitilafu za jamii hiyo, lakini serikali ya London haijachukua hatua zozote dhidi ya taasisi hizo za Kiyahudi. Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa, inachopaswa kufanya serikali ya Uingereza ni kuwasahilishia njia Waislamu wa nchi hiyo ya kufanikisha kiurahisi mahitaji yao na sio kuzibana na kuzisumbua taasisi zao ambazo zimeundwa kisheria. Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza amesema, hatua ya serikali ya David Cameron ya kuunda timu hiyo inalenga kuwatangazia walimwengu kuwa Waislamu ndio tatizo kubwa kwa jamii ya Uingereza, wakati ambapo jamii hiyo ina haki sawa na raia wengine wote wa nchi hiyo. Hatua hiyo ya serikali ya Uingereza imechukuliwa katika hali ambayo kundi la mrengo wa kulia lenye misimamo mikali nchini humo limetangaza habari ya kuanzisha kampeni maalumu yenye jina la "hatua ya moja kwa moja" kwa ajili ya kukabiliana na wanasiasa Waislamu waliochaguliwa na wananchi. Genge hilo lenye misimamo mikali linalojulikana kwa jina la Britain Frost ni la waungaji mkono wakubwa wa timu hiyo iliyoundwa na serikali ya Uingereza. Kampeni hiyo mpya iliyoanzishwa kwa lengo la kuwashinikiza Waislamu, inawalenga wanasiasa maarufu wa Uingereza kama vile Sadiq Khan, Meya wa jiji la London, Sajid Javid, Waziri wa Kazi, Muhammad al Taf Khan, Meya wa Oxford, Hussein Akhtar, Meya wa Black Bern pamoja na Shafiq Shah, Meya wa Birmingham. Kampeni hiyo imewataka wafuasi wake wawaite viongozi Waislamu nchini Uingereza kuwa ni wavamizi na wafuatilie kila nukta ya maisha yao. Kwa kweli vitendo vya kibaguzi dhidi ya Waislamu barani Ulaya ikiwemo Uingereza vimeongezeka baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 2015 mjini Paris Ufaransa, mashambulizi ambayo hadi leo yanaendelea kutumiwa vibaya na maadui wa Uislamu kueneza chuki dhidi ya Waislamu barani Ulaya. Tab'an kwa huko Uingereza na hasa njini London, uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, si Waislamu peke yao wanaokabiliwa na vitendo vya kibaguzi, bali watu wenye asili ya Afrika na wenye asili ya Asia wanalengwa sana na vitendo vya kibaguzi nchini humo, suala ambalo linazidi kubainisha ni namna gani Uingereza ilivyojaa misimamo ya kibaguzi, licha ya kujinadi duniani kuwa ni kinara wa kutetea haki za binadamu ulimwenguni.