“Huenda Trump akaitumbukiza Marekani katika vita vya pili vya ndani”
Mchambuzi mmoja wa masuala ya siasa amesema yumkini aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump akaitumbukiza nchi hiyo katika vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe.
Profesa Beau Grosscup, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Jimbo la California nchini Marekani ametahadharisha kuwa, nchi hiyo ipo katika hatari ya kutumbukia katika vita vya pili vya ndani, iwapo Trump na wafuasi wake wenye misimamo ya kuchupa mipaka hawatadhibitiwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika mahojiano na kanali ya Press TV, Profesa Grosscup amesema Trump na wafuasi wake mafashisti ni tishio kwa mfumo wa uchumi na siasa za Marekani, na wanapania kuleta utawala wa kimabavu nchini humo.
Ameongeza kuwa, “Kama ada, misimamo ya jeshi la Marekani itaamua si tu iwapo kutaibuka vita vya ndani au la, lakini pia ni nani atakayechaguliwa kuwa rais wa Marekani katika uchaguzi ujao.”
Matamshi ya Profesa huyo wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Jimbo la California yanakuja siku chache baada ya Trump kusema kuwa, iwapo atagombea na kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2024, atawasamehe na kuagiza kuachiwa huru watenda jinai waliohusika na shambulizi dhidi ya jengo la Kongresi mnamo tarehe 6 Januari mwaka jana, lililofanywa na wafuasi wake.
Watu wasiopungua watano wakiwemo maafisa usalama wa nchi hiyo waliuawa katika shambulio hilo la kutisha, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.