Taliban yatishia kuangalia upya sera za Afghanistan kwa Marekani
Serikali ya Taliban nchini Afghansitan imetishia kuangalia upya misimamo na sera zake kwa Marekani, iwapo Washington itakataa kuachia mabilioni ya fedha za Waafghani ilizozuilia.
Naibu Msemaji wa Taliban, Inamullah Samangani amesema, "Iwapo Marekani haitaachana na msimamo wake huo (wa kuzuia fedha za Afghanistan) na iendelee na hatua zake za kichochezi, basi Imarati ya Kiislamu (Serikali ya Taliban) pia italazimika kuangalia upya sera zake mkabala wa nchi hiyo (Marekani)."
Ameongeza kuwa, iwapo Marekani haitaki kukumbwa na ghadhabu za jamii ya kimataifa na kutoharibu uhusiano wake na taifa la Afghanistan, basi haina budi kufutilia mbali msimamo wake huo.
Ijumaa iliyopita, Ikulu ya White House ilitangaza kuwa utawala wa Joe Biden unapanga kuchukua kwa mabavu nusu ya dola bilioni saba fedha za Afghanistan zinazoshikiliwa katika benki za Marekani na kuzigawa kwa familia za walioathirika na mashambulizi ya Septamba 11 mwaka 2001.
Siku chache zilizopita wananchi wa Afghanistan walifanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, kulalamikia hatua hiyo ya Marekani ya kupora mabilioni ya dola za Afghanistan na kuzitenga kwa ajili ya kuwalipa Wamarekani wanaodai fidia kutokana na mashambulizi ya Septemba 11.
Serikali ya Taliban nchini Afghansitan imelaani vikali hatua hiyo ya kuporwa fedha za nchi hiyo ikisisitiza kuwa, wizi huo ni dalili ya kuporomoka maadili ya Marekani.