Kumairishwa ushirikiano wa kiusalama na kiintelijinsia kati ya Uturuki na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80470-kumairishwa_ushirikiano_wa_kiusalama_na_kiintelijinsia_kati_ya_uturuki_na_israel
Mgogoro wa kiuchumi na matatizo ya kifedha yanayoikabili Uturuki yameendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 17, 2022 23:14 UTC
  • Kumairishwa ushirikiano wa kiusalama na kiintelijinsia kati ya Uturuki na Israel

Mgogoro wa kiuchumi na matatizo ya kifedha yanayoikabili Uturuki yameendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya nchi hiyo.

Ukweli ni kuwa, wananchi wa Uturuki khususan wale walioathirika na hali hiyo mwaka jana walipitia tajiriba ya mgogoro mkubwa wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo. Kuhusiana na suala hilo, gazeti la Yeni Chagh la Uturuki toleo la Jumatano Februari 16 liliandika: Serikali ya Erdogan haina uwezo wa kuendesha nchi." Aidha habari kuu ya gazeti la Suzjo ilihusiana na suala hilo na kuandika: "Bidhaa zote zimepanda bei nchini na hali ya uchumi ni mbaya."

Vyombo vingine vya habari vya Uturuki pia vimeakisi pakubwa suala hilo. Radiamali hizo za vyombo vya habari vya Uturuki zinabainisha ukweli huu kwamba serikali ya Rais Recep Tayyep Erdogan haina uwezo wa kukabiliana na matatizo ya kifedha na mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo. Kushindwa serikali ya Erdogan kupunguza matatizo ya kiuchumi na mengine yanayowasibu wananchi wa Uturuki kumepelekea kupungua sana uungaji mkono wa wananchi kwa Rais huyo na chama tawala cha Uadilifu na Ustawi. Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki ana ghadhabu na haridhishwi na hali ya mambo ya nchi hiyo hivi sasa; na wakati mwingine amekuwa akichukua maamuzi ya kuwafuta kazi baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Ankara au wa taasisi za serikali. Mhanga wa karibuni wa kushindwa huko kwa Erdogan ni Mkuu wa Kituo cha Takwimu cha nchi hiyo ambaye amefutwa kazi. Katika mazingira kama hayo, inaonekana kuwa viongozi wa serikali ya Rais Tayyep Erdogan wa Uturuki wangali wanaendeleza siasa za undumakuwili na za kinafiki khususan katika kushirikiana na utawala wa Kizayuni ikiwa ni muendelezo wa sera za Ankara za kuibua mivutano na mikwaruzano katika uhusiano na nchi za eneo.

Bendera ya Israel

 

 Ni wazi kuwa viongozi wa serikali ya Uturuki ambao wamegonga mwamba kutokana na sera zao zilizofeli na zisizo sahihi katika kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo, wamejikita katika kuchukua hatua na maamuzi ya kustaajabisha kwa kudhani kuwa kuanzisha tena uhusiano na tawala za kidikteta za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi na utawala baguzi wa Israel kunaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo ya sasa ya kifedha na mgogoro wa kiuchumi wa ndani ya Uturuki. 

Inatupasa kusema kuwa, viongozi wa serikali ya Ankara kwa mara nyingine tena wameamua kutekeleza siasa hizo zisizofaa badala ya kuzirekebisha. Viongozi hao wa serikali ya Erdogan  ambao wakati mmoja walikuwa wakiwakosoa watawala wa Imarati kwa usaliti wao kwa taifa la Palestina kwa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel, sasa wenyewe wamejipanga katika safu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa kibaguzi.

Kuhusiana na hilo, "Ekrem Ekşi", mhadhiri wa chuo kikuu na mmoja wa wataalamu wakuu wa masuala ya kisiasa huko Uturuki, huku akikosoa misimamo ya kinafiki ya maafisa wa Ankara katika kujibu vitendo vya watawala wa UAE, katika mahojiano na Idhaa ya Kituruki ya Sauti ya Jamhiri ya Kiislamu ya Iran alisema: "Licha ya kuwa majibu ya serikali ya Erdogan kwa hatua ya Imarati ni majibu ya kupongezwa, lakini kwanza tunapaswa kuuliza kwamba je, Uturuki yenyewe itakata uhusiano na utawala wa Kizayuni au la?"

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, imekuwa wazi kutokana na swali hili la msingi la mtaalamu huyo mashuhuri wa Uturuki kwamba makele mengi ya viongozi wa Ankara, hasa ya Rais wa Uturuki dhidi ya Imarati na nchi zingine za Kiarabu za kiimla katika Ghuba ya Uajemi, yamekuwa ni ya kipropaganda tu yanayolenga kuhadaa na kupotosha fikra za waliowengi katika eneo.

Ni kwa msingi huo ndio vyombo vya habari vya Ankara hivi karibuni vikafichua ukweli kwamba viongozi wa Uturuki na utawala wa Kizayuni wamekuwa na uhusiano mkubwa wa kiusalama katika ngazi ya Idara ya Ujasusi ya Uturuki (MIT) na Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) katika miaka ya hivi karibuni. Kwa hakika, ushahidi uliopo unaonyesha kuwa uhusiano wa Uturuki na Israel umekuwa wa kawaida na unaendelea kupanuka. Kuhusiana na hilo, baadhi ya vyombo vya habari vya Uturuki vimenukuu vyanzo vya Israel vikisema: "Uhusiano wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) na Idara ya Ujasusi ya Uturuki (MIT) umeongezeka pakubwa katika miaka miwili iliyopita."

Mapatano ya nchi za Kiarabu kuimarisha uhusiano na utawala haramu wa israel

Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, uhusiano wa utawala wa Erdogan na Israeli unajumuisha uhusiano wa usalama na kiuchumi. Hatua ya maafisa wa serikali ya Erdogan inaonyesha kuwa serikali ya Uturuki imekuwa ikizua tu makelele ya ukosoaji dhidi ya nchi za Kiarabu na wakati huo huo kufanya makosa hayohayo yanayofanywa na nchi hizo kuhusiana na suala la kuimarisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.

Kwa maneno mengine ni kuwa, badala ya kukata uhusiano na Israel, viongozi wa Ankara wanaendelea kutekeleza siasa za undumakuwili na za kinafiki kuhusiana na utawala huo ghasibu na wa kibaguzi. Hatua hiyo haina maana nyingine ghairi ya kujaribu kuhadaa fikra za waliowengi nchini Uturuki na mataifa mengine ya Kiislamu duniani.