Marekani na NATO wahusika wakuu wa mzozo wa Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81526-marekani_na_nato_wahusika_wakuu_wa_mzozo_wa_ukraine
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema Marekani na NATO ndio wasababishaji wakuu wa mgogoro wa Ukraine na ndio wenye ufunguo wa kumaliza mgogoro huo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 18, 2022 15:30 UTC
  • Marekani na NATO wahusika wakuu wa mzozo wa Ukraine

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema Marekani na NATO ndio wasababishaji wakuu wa mgogoro wa Ukraine na ndio wenye ufunguo wa kumaliza mgogoro huo.

Zhao Lijian ameeleza kuwa, uamuzi wa Washington wa kulipanua Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuelekea Mashariki una uhusiano wa moja kwa moja na mgogoro wa sasa wa Ukraine.

Marekani ambayo ina wasiwasi kwamba China na kisha Russia zinahatarisha nguvu yake ya kibeberu duniani, inafanya juhudi kubwa ya kudhoofisha na kupunguza nguvu za madola hayo mawili. Kwa upande wa Russia, Marekani inajaribu kupanua eneo la udhibiti na shughuli za NATO hadi kwenye mipaka ya Russia, jambo ambalo limepingwa vikali na Moscow iliyozionya mara kwa mara Marekani na NATO kuhusu hatari ya jambo hilo na matokeo yake. Russia inaelewa vyema kwamba Marekani inazichochea nchi zinazoizunguka na zinazopakana nayo kujiunga na NATO kwa shabaha ya kuibana nchi hiyo kwenye mipaka yake na kuhatarisha usalama wake wa kitaifa, jambo ambalo halikubaliwi na Moscow; na jibu la Russia kwa jaribio la Ukraine la kujiunga na NATO ni katika mkondo huo. 

Jeshi la Russia nchini Ukraine

Ali Omidi, mhadhiri wa chuo kikuu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anasema: "Wakati Russia ilipoona kwamba Marekani na NATO hazisikilizi maonyo ya Moscow kuhusu uanachama wa Ukraine katika jumuiya hiyo ya kijeshi na zinataka kuiweka nchi hiyo chini ya mwamvuli wao kwa njia ya kuhatarisha usalama wa jiografia ya kisiasa ya Russia, ilichukua hatua, hivyo nchi hizo ziliamua kuibua mgogoro wa Ukraine."

Lengo lingine la Marekani katika kuibua mgogoro wa Ukraine ni kujaribu kutenganisha baina ya China na Russia. Marekani inatekeleza sera ya kuzusha hitilafu na mgawanyiko baina ya nchi hizo mbili kwa kutoa shutuma mbalimbali dhidi ya China, ikiwa ni pamoja na eti ombi la Moscow kwa Beijing kupewa silaha, na hata imeionya Beijing mara kadhaa kuhusu kukwepa vikwazo vya Russia vinavyohusiana na mgogoro wa Ukraine. Marekani inaelewa vyema kwamba, iwapo China na Russia zitaungana dhidi ya Magharibi, zinaweza kuvunja ubeberu na udhibiti wa Marekani kwa urahisi katika uwanja wa kimataifa. 

Maryam Khormaei, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema: "Moscow na Beijing zina mistari myekundu na zimeamua kuungana dhidi ya sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na za kulazimisha na kuwatwisha wengine demokrasia ya Kimagharibi na kuingilia mambo yao ya ndani, na hili linavuruga hesabu za Marekani."

Alaa kulli hal, hatua ya nchi za Ulaya, NATO na Marekani ya kutoisaidia na kuihami Ukraine imeithibitishia tena Kyie na washirika wengine wa nchi za Magharibi kwamba nchi hizo hazijali isipokuwa tu maslahi yao. Ndiyo maana Ukraine imefikia hitimisho kwamba imekuwa mwanasesere katika mikono ya NATO na nchi za Magharibi, jambo ambalo limesababisha gharama kubwa kwa watu wa Ukraine.