China: NATO inaiingiza dunia katika Vita Baridi
China imelionya Shirika la Jeshi la Nchi za Magharibi NATO dhidi ya kuitumbukiza dunia katika kipindi kipya cha Vita Baridi kupitia sera zake za usalama zilizopitwa na wakati.
Msemaji wa ubalozi wa China katika Umoja wa Ulaya mjini Brussels alitoa indhari hiyo jana Jumamosi kupitia taarifa na kueleza kuwa, "muungano mkubwa zaidi wa kijeshi duniani, NATO unafuata sera za kiusalama zilizopitwa na wakati."
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, NATO inapanua wigo wake wa kijiografia na operesheni za kijeshi kupitia mbinu za Vita Baridi, ili kuichochea miungano hasimu.
Msemaji wa ubalozi wa China katika Umoja wa Ulaya mjini Brussels ambaye jina lake halikutajwa ametahadharisha kuwa: Tunapaswa kuwa macho na tukatae Vita Baridi vipya.
Alkhamisi ya Machi 24, shirika la NATO liliituhumu China kuwa inaiunga mkono na kushirikiana na Russia katika mgogoro wa Ukraine.
Kikao cha dharura cha wakuu wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO kilichofanyika siku hiyo mjini Brussels, ilikuwa ni fursa nyingine kwa wakuu wa nchi za Magharibi ya kuzidi kuonesha msimamo wao wa kiuadui dhidi ya Russia na kupata kisingizio cha kushadidisha mgogoro wa Ukraine.