Ombi la wakazi asilia wa Canada kwa Papa Francis
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81902-ombi_la_wakazi_asilia_wa_canada_kwa_papa_francis
Wenyeji wa Canada walionusurika na mauaji ya shule za bweni za Kanisa Katoliki Jumatatu ya jana walimtaka Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani na mkuu wa Vatican, awezeshwe kupata kuona nyaraka zinazohusiana na jinai hiyo ya mauaji ya kimbari yaiiyolenga maelfu ya watoto wa Wahindu Wekundu na wakazi asilia wa Canada.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Mar 29, 2022 07:11 UTC
  • Ombi la wakazi asilia wa Canada kwa Papa Francis

Wenyeji wa Canada walionusurika na mauaji ya shule za bweni za Kanisa Katoliki Jumatatu ya jana walimtaka Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani na mkuu wa Vatican, awezeshwe kupata kuona nyaraka zinazohusiana na jinai hiyo ya mauaji ya kimbari yaiiyolenga maelfu ya watoto wa Wahindu Wekundu na wakazi asilia wa Canada.

Papa Francis alikutana kwa muda wa saa moja na wawakilishi wa makabila ya Metis na Inuit, na imepangwa kuwa atakutana na wawakilishi wa makabila mengine mawili ya Canada katika siku zijazo. Watu wa kabila la Metis wanataka kuoneshwa nyaraka na rekodi zote zinazohusiana na mauaji hayo zinazohifadhiwa na kanisa Katoliki.

Kuanzia mwaka 1883 hadi 1996 zaidi ya watoto laki moja na nusu wa wakazi asilia wa Canada walilazimishwa kuishi katika shule makhsusi za bweni zilizokuwa zikisimamiwa na wamishonari na wahubiri wa Kikatoliki. 

Lengo kuu la kutekelezwa mradi huo lilikuwa kuwatenganisha watoto hao na jamii zao asili za Canada ili kuwazuia kujifunza lugha, mila na desturi zao. Watoto hao walikumbwa na masaibu chungu nzima ambapo wengi waliteswa, kunajisiwa na kudhalilishwa kingono wakiwa katika shule za washonari wa Kikatoliki. Kutokana na hali hiyo baadhi ya watoto walipoteza maisha msimu wa baridi wakiwa jangwani wakijaribu kutoroka hali mbaya shuleni. 

Watoto wa wakazi asilia wa Canada

Mtandao wa gazeti la The National Post la Canada uliripoti kwamba, kumegunduliwa mamia ya makaburi ambayo hayajasajiliwa katika mkoa wa Saskatchewan ambayo yanadhaniwa yana maiti za watoto waliokuwa wakishikiliwa katika shule nyingine ya bweni ya wamishonari wa Kikatoliki. Makaburi hayo ambayo hayana alama yoyote yana maiti za mamia watoto wa wakazi asilia. Kugunduliwa makaburi hayo kumezusha mshtuko mkubwa nchini Canada na maeneo mengine ya dunia. Kwa sasa zinafanyika jitihada za kusaka makaburi mengine ya aina hiyo.  

Rosanne Casimir ambaye ni mkuu wa mojawapo ya makabila ya mji wa Kamloops katika jimbo la British Columbia alisema baada ya kugunduliwa makaburi hayo mwaka jana kwamba: "Vifo vya watoto hao wa wakazi asilia wa Canada havikusajiliwa katika waraka wowote wa shule, na suala hili pekee ni ushahidi kwamba, maafisa na viongozi wa shule hizo walihusika katika vifo vya watoto hao."

Tangu mwezi Mei mwaka jana kumegunduliwa maeneo kadhaa yenye makaburi ya miili ya watoto hao wa shule za bweni za huko British Colombia, Saskatchewan na Manitoba. Mabaki ya miili ya watoto wasiopungua 1148 imepatikana katika kaburi la umati na makaburi mengine kadhaa yasiyo na majina ya watoto waliozikwa ndani yake. 

Ripoti ya Kamati ya Ukweli na Maridhiano ya mwaka 2015 imeonyesha kuwa, watoto wasiopungua 4,100 waliuliwa wakiwa katika shule za bweni za Wamishonari wa Kikatoliki au kutoweka. 

Kanisa Katoliki na Serikali ya Canada, wamechangia pakubwa katika unyanyasaji na ukatli dhidi ya watoto wa wenyeji na wakazi asili katika karne za hivi karibuni kwa kuanzisha na kuendesha mamia ya shule za watoto waliotenganishwa kwa nguvu na familia zao. 

Wenyeji wa Canada ndio walikuwa wakazi asilia wa ardhi hiyo kabla ya kugunduliwa Marekani kwenye karne ya 15 na bado wanaishi ndani ya mipaka ya Canada ya leo wakijumuisha makabila ya awali ya Inuit na Metis. 

Takwimu zinaonesha kuwa, Canada ina zaidi ya Wahindi Wekundu milioni moja na laki mbili, na jamii yao inaishi katika hali mbaya ikisumbuliwa na kiwango cha juu ya umaskini, kujiua na uraibu wa dawa za kulevya. Hii ina maana kwamba, jamii hiyo ya wenyeji inasumbuliwa na matatizo mengi yanayotokana na siasa za ubaguzi wa kimbari za serikali ya Canada. Watu wa jamii hii wamekuwa wakiishi katika sulubu na ukandamizaji mkubwa wa wazungu na serikali ya Ottawa kwa karne kadhaa sasa.

Mojawapo ya mifano ya wazi zaidi ya unyama na ukatili wa kutisha uliofanywa kwa wakazi hao asilia ni makumi ya makaburi ya halaiki ya watoto wa wakazi asilia yaliyogunduiwa katika maeneo mbalimbali nchini Canada hususan maeneo ya shule za bwezi za wamishonari wa Kikatoliki. Watoto hao walikuwa wakitenganishwa kwa mabavu na wazazi wao na kupelekwa kwenye mabweni ya shule za kanisa Katoliki ili kutekeleza sera za serikali ya Canada ya kufuta utamaduni na utambulisho wa wenyeji na badala yake kueneza utamaduni wa wahamiaji wazungu. Kugunduliwa kwa makaburi haya ya umati ni ukumbusho wa jinsi Wacanada asilia walivyokumbana na ubaguzi wa kimfumo tangu baada ya wazungu kuvamia na kuhamia Amerika Kaskazini; na hali hiyo ingali inaendelea. 

Japokuwa Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amefanya jitihada za kufunika fedheha ya kugunduliwa mamia ya makaburi ya umati yenye maelfu ya maiti za watoto wa wenyeji hao kwa kuwapa watu wa jamii hiyo aina flani ya mamlaka, lakini ukweli ni kuwa jinai hiyo ni kubwa mno na imekita mizizi katika historia ya Canada kiasi kwamba, si rahisi kuifuta kwa hatua kama hizo za kipropaganda.

Justin Trudeau

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wenyeji wa Canada, Perry Belgerd ameashiria ukweli huo mchungu akisema kuwa kugunduliwa makaburi ya umati ya wanafunzi wa shule za bweni za wamishonari nchini Canada si jambo jipya na kwamba ni jeraha la miaka mingi ambalo kufunuliwa kwake daima huambatana na maumivu makali.

Mienendo ya kibaguzi ya serikali ya Canada dhidi ya wenyeji na wakazi asili wa nchi hiyo imeendelea pia katika karne ya 21 na kukabiliwa na upinzani mkubwa wa mashirika na jumuiya za kutetea haki za binadamu. Ripoti ya karibuni ya shirika la Amnesty International ilitangaza kuwa, kuwatenga na kutowashirikisha wakazi asili na wenyeji wa Canada katika uchukuaji wa maamuzi ya nchi kunaifanya Canada iwe mbali na vigezo vya haki za binadamu vilivyotangazwa katika Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wakazi asilia na wenyeji.

Ripoti iliyotolewa mwaka 2018 na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa iliashiria vipengee vya kibaguzi vilivyoko katika “Sheria ya Wenyeji” (Aboriginal Law) nchini Canada. Ripoti hiyo imesema kuwa, Canada inapaswa kufuta vipengee hivyo vya kibaguzi. Sheria hiyo ilibuniwa mwaka 1876 kwa misingi ya ubaguzi.

Haya yote na licha ya kuwa, Canada imekuwa ikijigamba kuwa mtetezi wa haki za binadamu na daima imekuwa ikijitokeza katika majukwaa ya kimataifa kama Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuzituhumu nchi inazopinga sera za kibeberu za Wamagharibi.

Alaa kulli hal, faili la haki za binadamu la Canada lina nukta nyingi za giza ikiwa ni pamoja na mienendo ya kikatili ya serikali ya nchi hiyo dhidi ya wenyeji na wakazi asili.