Apr 26, 2022 07:40 UTC
  • Russia yaonya kuhusu uwezekano wa kutokea Vita vya Tatu vya Dunia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameonya kuwa, hivi sasa kuna uwezekano walimwengu wakashuhudia kutoka Vita vya Tatu vya Dunia.

Sergeĭ Viktorovich Lavrov amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na waandishi wa habari wa Russia na kuwalaumu viongozi wa Ukraine kwa kudharau nia njema iliyooneshwa na Moscow kuhusu mazungumzo.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Russia amemshutumu pia rais wa Ukraine kwa kujifanya anapenda na mazungumzo na kuongeza kuwa, rais huyo ni mcheza filamu mahiri lakini unapoangalia kwa kina kile anachokisema utaona kuna maelfu ya migongano katika matamshi yake.  Vita vya Ukraine vimeingia katika mwezi wake wa tatu na hasara zinaendelea kushuhudiwa katika pande zote mbili. 

Ukraine imepata hasara kubwa katika vita, lakini viongozi wapenda Umagharibi wa nchi hiyo wanaendelea kukaidi mazungumzo

 

Jumamosi iliyopita pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov alisema kuwa, mazungumzo baina ya Moscow na Kyiv yamekwama. Alisema, licha ya kupita siku tano za mapendekezo ya Russia kwa Ukraine, lakini Kyiv ilikuwa haijatoa majibu yoyote na alisisitiza kwa kusema: Mimi ninadhani kwamba viongozi wa Ukraine hawana nia ya kuendelea na mazungumzo hayo.

Tangu vilipoanza vita vya Ukraine tarehe 24 Februari mwaka huu, kumeshafanyika mazungumzo kadhaa baina ya wajumbe wa Russia na Ukraine lakini yote yameshindwa kuleta usimamishaji vita wa pande zote.

Vita vya Ukraine havioneshi ishara zozote za kumalizika hivi karibuni kutokana na nchi za Magharibi kuzidi kuchochea vita hivyo na kuilazimia Russia ichukue hatua za kujihami kama uamuzi wake wa kuweka makombora yake mapya ya masafa marefu ya Sarmat, ambayo yana uwezo wa kuanzisha mashambulizi ya nyuklia dhidi ya Marekani.

Tags